Baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Juliet
Kairuki, mjadala umeibuka kuhusu kitendo cha mkurugenzi huyo mtendaji wa
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kutochukua mshahara tangu mwaka
2013 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Kitendo hicho kimetajwa kuwa moja ya sababu za kutimuliwa kwake.
Swali hilo na sababu tofauti za uamuzi huo ndizo zilizotawala
mijadala mbalimbali kwa siku nzima ya jana, ikiongozwa na mitandao ya
kijamii.
Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa kutengua uteuzi wa Kairuki
Alhamisi ya jana akisema uamuzi huo ulifanywa tangu Aprili 24 na kwamba
moja ya sababu za kuondolewa kwake ni kutochukua mshahara tangu Aprili,
2013.
“Pamoja na mambo mengine, hatua hii imechukuliwa baada ya Mheshimiwa
Rais kupata taarifa kuwa Bibi Kairuki amekuwa hachukui mshahara wa
Serikali tangu alipoajiriwa Aprili 2013 mpaka sasa, jambo linalozua
maswali mengi,” inasema taarifa ya Profesa Adolf Mkenda, katibu mkuu wa
Biashara na Uwekezaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Tofauti na watumishi wengine waandamizi ambao baada ya uteuzi wao
kutenguliwa Ikulu ilisema watapangiwa kazi nyingine, kwa Kairuki
atapangiwa kazi nyingine iwapo atataka kuendelea kufanya kazi
serikalini.
Awali ilishawahi kuripotiwa katika vyombo vya habari kuwa Kairuki
alikuwa hachukui mshahara uliotajwa kuwa Sh5 milioni (ambao Mwananchi
haijaweza kuthibitisha) unaotolewa na TIC kwa kuwa ni mdogo kulinganisha
na aliokuwa akipata nchini Afrika Kusini kabla ya kuombwa na Rais wa
Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuja nchini kusaidia kusukuma
gurudumu la maendeleo.
Kabla ya kuteuliwa na Kikwete kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na
Emmanuel Ole Naiko kustaafu, Kairuki alikuwa akifanya kazi Afrika Kusini
katika chama cha benki cha Afrika Kusini, akiwa meneja mkuu wa Idara ya
Benki na Huduma za Fedha.
Inadaiwa kuwa akiwa TIC, Kairuki, ambaye ni mwanasheria alikuwa
akipendekeza apewe mshahara wa Sh18 milioni kwa mwezi kiwango ambacho
kinadaiwa kingeendana na stahiki alizokuwa akipata Afrika Kusini. Madai
hayo yalipingwa na Kairuki mwaka jana.
Katika mjadala mwingine, inaelezwa kuwa pamoja na kutolipwa
mishahara, Kairuki aliweza kumudu maisha kutokana na kuwa na safari
nyingi zinazoendana na nafasi yake ya kuweka mazingira mazuri ya
uwekezaji na hivyo kupata posho nzuri.
Kundi jingine lilieleza kwenye mijadala hiyo kuwa Kairuki alikuwa
akilipwa posho zinazofikia Sh25 milioni na hivyo kuweza kumudu maisha
bila ya kuchukua mshahara.
Hakuna mjadala ulioweza kuthibitisha madai hayo, lakini imeelezwa
kwenye mitandao hiyo kuwa hali iligeuka baada ya Serikali kukubaliana
naye mshahara na mtendaji huyo kudai malimbikizo yote ya mishahara
ambayo hakulipwa.
Jitihada za kumpata Kariuki jana ziligonga mwamba.
Profesa Mkenda hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo la mshahara na mtumishi wake wa zamani.
“Mshahara wa nafasi hiyo upo na umekuwepo siku zote. Kabla yake kulikuwa
na mtangulizi wake alikuwa anapokea mshahara,” alisema Profesa Mkenda
kupitia ujumbe mfupi wa simu.
Alipoulizwa ni jambo gani lilitokea hadi Kairuki asichukue mshahara
huo na Serikali ilichukua hatua gani za awali kumalizana naye mapema
kabla ya kumalizika miaka mitatu, Profesa Mkenda hakujibu ujumbe wa
swali hilo.
Lakini alisisitiza kuwa ngazi ya mshahara ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC
ipo na haijawahi kubadilishwa tangu taasisi hiyo ianzishwe.
Hata hivyo, mwandishi wetu alipotaka ufafanuzi kutoka kwa katibu mkuu
huyo iwapo mshahara ulikuwa ukiingia katika akaunti ya Kariuki halafu
hautumii au haukupelekwa kabisa katika akaunti yake, hakujibu.
Katibu Mkuu Wizara ya Utumishi, Dk Laurian Ndumbaro alisema jambo
hilo alikuwa amelisikia kwa mara ya kwanza mchana na kueleza kuwa
Profesa Mkenda ana majibu zaidi.
Alipoombwa kuelezea iwapo kanuni au taratibu za utumishi zinambana
mtu asiyechukua mshahara, aliahidi kumtafuta mwandishi kwa kuwa alikuwa
bungeni lakini baadaye hakupokea tena simu.
Watu waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Damian Shumbusho alisema iwapo alitenguliwa bila
uchunguzi wa kina, uamuzi huo si wa busara.
Alisema kuwa iwapo kukubali kufanya kazi pasipo kuchukua mshahara ni
kosa kwake na Serikali nayo inawajibika kwa kuwa Sheria ya Ajira na
Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004 hairuhusu mtu kufanya kazi kabla ya
makubaliano. “Hapa tatizo linaonekana lipo kwenye mkataba. Pasipo
makubaliano ya mshahara mtu hawezi kufanya kazi,” alisema Shumbusho.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Nicholas Mgaya alionyesha wasiwasi wa mwajiriwa kutochukua mshahara.
“Unakula nini siku zote kama huchukui mshahara? Kwanini huchukui
mshahara wako na kuutumia. Una kula rushwa au una chanzo kingine cha
mapato kisichojulikana?” alihoji.
Alisema Tucta hawawezi kuzungumzia jambo lolote linalohusu wateule wa
Rais kwa kuwa ana mamlaka kikatiba kutengua uteuzi wao, lakini wana
uhakika Dk Magufuli alifanya uchunguzi wa kina na kushauriwa na
wataalamu kabla ya hatua ya jana.
Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu, Elias Baraka kama wengine
alihoji Kairuki alikuwa akiishi vipi bila kuchukua mshahara na kama
uchunguzi umebaini hivyo ana tatizo la kukwepa uwazi.
“Kama uchunguzi umefanyika na ukabaini hivyo, ana kosa la kutokuwa
mwaminifu. Hakuwa muwazi. Alikuwa anaishije bila mshahara? Hivyo adhabu
hiyo itakuwa sahihi vinginevyo alitakiwa asimamishwe kwa uchunguzi
zaidi,” alisema Baraka.
Wakati Profesa Mkenda akitangaza utenguzi huo, Kairuki alitakiwa kuwa
mmoja wa waongozaji wa mkutano wa wawekezaji kutoka Urusi uliokuwa
ukiendelea jana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius
Nyerere.
Kairuki, ambaye taasisi yake ilikuwa moja ya waandaji wa mkutano huo,
hakuonekana tangu asubuhi hata kabla ya tangazo la kutumbuliwa. Ratiba
ya mkutano huo inaonyesha kuwa alitakiwa kuongoza mkutano huo muhimu
sambamba na mwanzilishi wa kampuni ya b2b-export.com kutoka Urusi,
Ekaterina Dyachenko na kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji
Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage a
aliyekuwepo katika mkutano huo, alipoulizwa kuhusu sababu ya Kairuki
kutopokea mshahara na sababu za Serikali kutochukua hatua kwa miaka
aliyotumikia TIC, alisema hakuwa na taarifa za kutimuliwa kwa Kairuki.
“Hii ni habari (mpya) kwangu. Nimefika kutoka bungeni asubuhi hii,” alisema.
Source: Mwananchi
0 comments: