Bahati lusambo: Local News

Sunday, 28 August 2016

Profesa Lupumba,Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya Wavuliwa Uanachama CUF

Chama Cha Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya.

Uamuzi huo umetolewa jana na Baraza Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake visiwani Zanzibar kwa lengo la kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kabla ya kusimamishwa.

Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua.

Mbali na vigogo hao, wengine waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee, Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya.

Aidha, Baraza hilo limemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. Hatua hii inaweka matatani ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Lipumba na Sakaya hawakupata nafasi ya kujitetea kutokana na kutohudhuria mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi ya kujitetea kutokana na uwepo wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda. Katiba ya chama hicho haiwapi nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Baraza hilo.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku chacha baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliolenga kumchagua Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo vurugu kubwa baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na wafuasi wake wakitaka barua yake ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake ijadiliwe na kukubaliwa.

Hata hivyo, kura zilizopigwa na wajumbe wote zaidi ya 800, ni kura 14 pekee zilizotaka Profesa Lipumba aendelee na nafasi ya uenyekiti.
Askari Magereza Atiwa Mbaroni Kwa Kuingia Wodini Akiwa Amelewa na Kisha Kuanza Kufyatua Risasi


POLISI mkoani Rukwa inamshikilia askari Magereza, Cleophas Chapaulinge kwa kosa la kulewa na kupiga risasi hewani akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga na kusababisha taharuki kubwa kwa wagonjwa na wauguzi.

Kitendo cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba tisa ya wanawake na watoto, ambapo akinamama walipiga mayowe kwa hofu huku wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha watoto wao vitandani.

Akizungumza  kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha kutokea kwa tukio hilo  na kueleza kuwa lilitokea jana alfajiri.

“Chanzo ni ulevi wa kupindukia tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha kipimo ni alama kati ya 70 na 40 …. Katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10,” alisema.

Kamanda Kyando alisema siku ya tukio, askari huyo akiwa na mwenzake walikuwa kwenye lindo akilinda makazi ya Kamanda wa Magereza wa Mkoa, lakini alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba tisa, ambako mkewe alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.

Mke wa mtuhumiwa huyo, Theresia Kalonga ambaye naye ni askari Magereza, alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.

“Mtuhumiwa huyo tunamshikilia huku taratibu za kumkabidhi kwa Kamanda wa Magereza Mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea,” alisisitiza Kamanda Kyando.

Akizungumza hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha alisema askari huyo baada ya kuingia wodini, aliweka silaha yake chini akafunua chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje na kufyatua risasi hewani na kutoboa paa.

“Mtuhumiwa huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa,” alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa hospitalini hapo na mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa, lakini alisababisha taharuki kubwa hospitalini.

“Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwahi kufika hospitalini hapo na kumtia nguvuni, na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa ikiwa na risasi kumi,” alisema.

Muuguzi wa zamu wodini humo, Rose Katabi alisema askari huyo alipofyatua risasi akinamama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha muuguzi kwa ajili ya kusalimisha maisha yao.

“Kwanza kitendo cha kumuona askari huyo akiwa na silaha mkononi, mwili wangu wote ulikufa ganzi nilihisi atatulipua kwa kutupiga risasi za moto …aliiweka silaha yake hiyo chini na kuanza kuzungumza na mwanawe. Aliniuliza kama mtoto wake ameshakunywa dawa, nikamjibu anakunywa dawa mara moja usiku.

“Waliingia walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza, kusema atarudi tena, akatoka nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua risasi hewani iliyotoboa paa kisha akaondoka na kutokomea gizani,” alisema.

Kwa upande wa mke wa mshtakiwa huyo, Theresia alisema alipomuona na sare za jeshi na silaha mkononi alimtaka arudi mara moja kazini. 
Walinzi waliokuwa kwenye lindo katika lango kuu la kuingia hospitalini hapo kwa masharti ya kutoandikwa majina yao , walidai kuwa askari huyo alifikishwa hospitalini hapo kwa usafiri wa bodaboda.

“Alitutia shaka baada ya kukataa kusimama, kwani alipitiliza moja kwa moja akiwa na silaha mkononi, tulijawa na hofu kubwa tukaamua kumfuata kwa nyuma hadi akaingia wodi namba tisa alikolazwa mkewe na mtoto wake. Lakini tulipomuona akikoki bunduki yake tulilazimika kukimbia na kwenda kujificha ndipo tukasikia mlio wa risasi,” alisema mmoja wao.
Godbless Lema Agoma Kula Kwa Saa 48


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ( Chadema) anayeshikiliwa katika mahabusu ya kituo kikuu cha Arusha Mjini amegoma kula kwa zaidi ya saa 48 sasa tangu alipokamatwa

Lema alikamatwa juzi alfajiri akiwa nyumbani kwake Njiro Arusha kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi  na kushawishi watu kwa njia ya mtandao waandamane Septemba mosi.

Jana Meya wa Arusha, Calist Bukhay alisema Lema amegoma kula

Alisema Lema aligoma kula akidai kuwa alifanyiwa udhalilishaji mbele ya watoto wake wakati polisi walipokuwa wakitekeleza agizo la kumkamata.

"Ni kweli amegoma kula tangu jana (juzi) alipokamatwa.Alisema askari polisi walipkwenda kumkamata walimfanyia vitendo vya udhalilishaji mbele ya watoto wake na kumnyanyasa bila kujali yeye ni kiongozi wa wananchi.

"Sasa  yeye ameshikilia msimamo wake kuwa kwa kuwa polisi walikuwa wamepanga kumuua wakati wa kumkamata, basi ni bora akafa kwa njaa.

"Chakula kimekuwa kikipikwa na kupelekwa na mkewe ,lakini bado amegoma kukila.Baada ya tukio hilo, polisi walituita ili kujaribu kumshawishi ale mchana, akagoma" Alisema Meya Calist.

Thursday, 25 August 2016

Mtoto aliyepotea akutwa chooni akiwa amefariki,huku akiwa na jamaa wa jirani



Huzuni imetanda katika mtaa mmoja wa Tabata jijini Dar es salaam baada ya mtoto wa miaka 3 kufariki katika mazingira ya kutatanisha.Mtoto huyo ambaye ni wakiume alipotea  na baada ya kutafutwa  sanaa alikuja kupatikana chooni akiwa na jamaa mmoja huku mtoto akiwa hana nguo.
Wananchi walianza kumshushia kipondo jamaa huyo mkatili kabla ya kumpeleka polisi huku mtoto akikimbizwa hospitali bila kujua kwamba tayari alikuwa ameshafariki.

Uchunguzi wa daktrai ulionyesha kuwa hakuna kitu chochote kibaya ambacho mtoto alichofanyiwa lakini inasemekana njemba hilo lilimkaba mtoto ili asipige kelele.
Huzuni imetanda mtaani hapo huku wazazi wakiwa nahofu kubwa kwa watoto wao hata kuwaruhusu kwenda nje kucheza wanaogopa.Kinachoumiza zaidi ni kwakuwa jamaa huyo ni wa hapohapo mtaani na watu wanamjua.


CHADEMA Wapinga Kauli ya Jeshi la Polisi Kuzuia Mikutano ya Ndani ya Vyama vya Siasa

Wakati Jeshi la Polisi likisisitiza kupiga marufuku mikutano na maandamano ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (Ukuta), chama hicho kimepinga katazo hilo nakudai kuwa ni haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao Makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, jijini Dar es Salaam.

Kwenye mkutano huo akiwa na Lawrance Masha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani (2005-2010) Lissu amesema, rais anayo nafasi ya kuzuia mikutano ya hadhara kwa sharti la kupeleka hoja bungeni na kisha kujadiliwa na si vinginevyo.

“Ipo sheria ya kutangaza hali ya dharura, iliyotungwa mwaka 1995, hii inamruhusu rais kupeleka hoja bungeni ya kutaka kutangaza hali ya dharura kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu na kama Bunge likiridhia, basi rais anatangaza, namshauri Magufuli afanye hivyo.

“Aitangazie Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa, nchi hii ipo katika hali ya hatari na katika hali ya dharura, na kwamba mikutano yote itakuwa marufuku.

“Na miezi mitatu ikiisha aende tena bungeni kuomba aongeze mingine. Akifanya hivyo atakuwa hajavunja sheria na hata sisi tutamtii,” amesema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutoa matamko yanayoiingiza nchi katika utawala wa kidikteta.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tu, tangu jeshi hilo kupitia Nsato Marijani, Kamishina wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, litangaze kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa nchini, ikiwemo vikao vya ndani vya vyama.

Katika mkutano na wanahabari, makao makuu ya chama hicho, akiwa ameambatana na Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu, pamoja na Masha amesema, Lissu amesema, kamwe Chadema hakiwezi kuruhusu ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.

“Amri ya jana ya polisi, wakipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa ikiwemo vikao vya ndani ni muendelezo wa amri haramu na kitendo hicho cha jana na vingine vilivyopita, ni mfano hai ya kwamba, nchi yetu imeingia katika mfumo wa udikteta.

"Kwani, kwa mujibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967; udikteta ni utawala wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache wanaofikiria kwamba, amri zao ndiyo sheria na wote wanaowapinga, hukiona cha mtema kuni,” amesema Lissu.

Lissu amesema kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya sasa pamoja na sheria zote ikiwemo Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, Sheria ya Maadili ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2007 pia sheria za Jeshi la Polisi, hakuna mahali ambapo polisi au rais anaruhusiwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.

“Anayetakiwa kujulishwa kuhusu uwepo wa maandamano na mikutano ya hadhara ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na kama kuna tatizo kwa muda huo, anaweza kuelekeza isifanyike kwa muda fulani lakini siyo Rais Magufuli wala Nsato,” amesema.

Wakati Lissu akisema hayo, Masha amesema, “nimekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miaka mitano, lakini sikuwahi kupiga marufuku mikutano ya hadhara wala ile ya ndani. Nilifahamu kuwa, kuna umuhimu wa watu kuzungumza, kukosoana na kuelimishana.

"Ni vyema Rais Magufuli akajua, hii ni nchi ya kidemokrasia na kuna Katiba na sheria ambazo kila mtu ni lazima afuate akiwemo yeye, matamko ya kibabe ya Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la polisi ni kinyume na sheria pamoja na Katiba yetu.”

Dk. Mashinji, amesisitiza kuwa, Chadema kipo tayari kwa mazungumzo na mamlaka yoyote ya serikali juu ya azma ya kufanya mikutano na maandamano, ili mradi tu sheria na katiba ya nchi izingatiwe katika mazungumzo hayo.

“Hatujafunga milango ya mazungumzo na serikali, tunachosisitiza sisi ni kuwa hata kama kuna mazungumzo yatafanyika, Katiba na sheria za nchi yetu lazima zizingatiwe,” amesema Dk. Mashinji.

Wednesday, 24 August 2016

Jeshi La Polisi Lahusisha Mauaji ya Polisi Wanne na Sakata la Oparesheni UKUTA.........Lapiga Marufuku Mikutano yote ya Ndani ya Vyama vya Siasa
KUFUATIA mauaji ya askari wanne yaliyotokea Kata ya Mbande Temeke kwa watu wanaodhaniwa ni majambazi kuvamia benki ya CRDB na kuwaua askari hao kwa kutumia silaha za moto jeshi la Polisi limetangaza kiama na kuwataka wahusika wote kujisalimisha.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi limehusisha tukio hilo na Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) kufuatia matamko ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha wafuasi wao wawashambulie askari wa Jeshi la Polisi.

Kauli hiyo imetolewa  na Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Nsato Marijan Mssanzya (CP), wakati akizungumza waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana ambapo pia alikiri kuwa mazoezi yanayofanywa na polisi yamelenga kukabiliana na Ukuta.

Akizungumza kwa hisia CP Mssanzya pia amepiga marufuku  mikutano ya ndani yenye viashiria vya uchochezi na hata ikifanyika kwenye majukwaa watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa sheria.

Amesema Jeshi  hilo limebaini kwamba mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuchochea wananchi na kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi na kufanya mapambano na jeshi la polisi

"Kwasababu hiyo basi,kwa hali ya kutumia mikutano ya ndani kuchochea watu kuvunja sheria na kupambana na askari, hivyo basi kuanzia sasa jeshi la polisi nchini linapiga marufuku mikutano yote ya ndani" amesema.
 
Aidha CP  Mssanzya  aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo wakati wakibadilishana lindo kuwa ni  E.5761 CPL Yahya, F.4660 CPL Hatibu, G 9524 PC Tito na G 9996 PC Gastoni na raia wawili waliojeruhiwa aliowataja kuwa Ali Chiponda na Azizi Yahya wote wakiwa wakazi wa Mbande.

"Katika tukio hilo majambazi ambao idadi yao haikufahamika walifanikiwa kupora silaha mbili aina ya MSG na lisasi 60 na hakuna pesa wala mali ya benki hiyo kuibiwa au kuharibiwa, ni dhahiri kuwa waharifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambiulia askari polisi, " alisema.

Alisema katika hali ya kushangaza baada ya tukio hilo kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukeji mazoezi ya kawaida ya jeshi la polisi na wengine waliandika ujembe wa kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari polisi huku wengine wakidiriki kuandika ujumbe unaosema endapo watapigwa na polisi Septemba1 mwaka huu basi viongozi wa jeshi hilo wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi limejipanga vyema kukabiliana na matukio yote ya uvunjifu wa amani nchini.
Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.

Atakayevamia Msitu Faini Mil. 70, Jela Miaka Saba- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili ambao ndiyo chanzo pekee cha maji cha Wilayani Nkasi atatozwa faini ya sh. milioni 70 pamoja na kifungo miaka saba jela.

Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa Waziri Mkuu amemkabidhi mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mtanda kitabu cha sheria kitachomuangoza katika kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya uharibifu katika chanzo hicho cha maji.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa mji Mdogo wa Namanyere katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanya vya Sabasaba.

“Mkuu wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua za kuwaondoa wananchi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi za misitu na kuanzisha makazi au kufanya shughuli za kijamii naye atakuwa jipu,” alisema.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji baada ya wananchi kuvamia katika vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu hivyo kusababisha vyanzo vingi kukakuka

“Serikali haitakubali kuona mtu anaharibu chanzo cha maji. Wananchi mnatakiwa kuwa walinzi wa maeneo hayo na atakayekutwa anachunga mifugo, analima, kukata nyasi au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya maeneo hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Awali Waziri Mkuu alikagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji Mfili ambalo mwanzo lilikuwa na ujazo wa lita 1,500 ambapo litakapokamilika litakuwa na ujazo wa lija 248,067 hivyo kuwezesha wakazi 82,689 kunufaika.

Akizungumza kwenye eneo la mradi mara baada ya Waziri Mkuu kuwasili, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo alisema hadi kukamilika mradi huo unatarajiwa kugharimu sh trilioni 1.011 ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetoa sh. milioni 500 na OOfisi ya Rais TAMISEMI itatoa sh. milioni 500.

Mkurugenzi huyo alisema mradi unakabiliwa na changamoto ya ukosefu umeme ppamoja na mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya umeme, ambapo aliiomba Serikali kuipatia halmashauri hiyo sh. milioni 222.576 ikiwa ni gharama za kupeleka umeme kwenye eneo la mradi na kununua mitambo.

Mbali na kutembelea mradi wa upanuzi wa bwawa, pia Waziri Mkuu alitembelea hospitali teule ya wilaya ya Nkasi na kuzindua wodi mpya yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 72 kwa wakati mmoja

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, JUMATANO, AGOSTI 24, 2016.
Utata kuhusu mashahidi wagubika kesi ya Tundu Lissu, yaahirishwa hadi Sept 6, mwaka huu.


Mvutano kuhusu maelezo ya mlalamikaji katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, baina ya mawakili wa upande wa  mashtaka na upande wa utetezi ulikwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Anadaiwa kuwa Juni 28, mwaka huu, Lissu akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa:
 
“Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.’’

Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa leo kwa upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi.Wakili wa Serikali Bernard Kongola aliieleza mahakama kuwa walikuwa na mashahidi wawili ambao aliwataja kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Staff Sajenti Ndege.

Hata hivyo kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala aliiomba mahakama wapewe maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo kabla ya kufanya jambo lolote, jambo ambalo liliibua mvutano wa hoja baada ya kupingwa na upande wa mashtaka.

Wakili Kongola aliieleza mahakama kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, si miongoni mwa mashahidi wao wanaokusudia kuwaita mahakamani.

Pia alisema kuwa kwa mujibu wa sheria hawalazimiki kutoa maelezo hayo ya mlalamikaji kwa mtu ambaye si shahidi.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai kuwa taarifa ya huyo mlalamikaji ndio chanzo au iliyosababisha kesi hiyo na kwamba iwapo watamleta au hawatamleta lakini maelezo yake ni sehemu ya kesi hiyo.

Alidai kuwa hata mashtaka yaliyopo chini ya sheria ya magazeti ni ya muhimu na kwamba hawawezi kujitetea bila kuyaona  na kwamba hata kama upande wa mashtaka hautamuita, wao wataiomba mahakama aitwe kwa lazima.

Hivyo aliiomba mahakama iulazimishe upande wa mashtaka uwapatie maelezo hayo ya mlalamikaji.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Dk Yohana Yongolo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu, atakapotoa uamuzi, baada ya kupitia vizuri hoja za kisheria za pande zote.

Tuesday, 23 August 2016

AUDIO ,Madawati yamfanya Waziri Mwinyi kutoa siku saba kwa halmashauri, majimbo
April 11 2016 Serikali ilitoa zabuni kwa JKT kutengeneza madawati 60,000 kwa gharama ya Bilioni 3 ambapo bei ya kila dawati ni sh 50,000/, aidha July 13 2016 JKT ilikabidhi madawati 32,387.
Leo August 23 2016 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amekutana na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa katika awamu ya pili madawati 20,000  yameshakamilika na yanaweza kuchukuliwa kuanzia sasa kwenda kwenye majimbo yaliyopangiwa kupata madawati hayo.
Katika kutekeleza mpango huo, awamu ya kwanza jumla ya madawati 32,387 yalitengenezwa na yaliyochukuliwa na Wabunge kwa kushirikiana na Halmashauri zao ni 22,721 tu, hivyo madawati 9,666 sawa na asilimia 30% bado hayajachukuliwa na Majimbo husika.
Akizungumzia Majimbo ambayo hayajachukua madawati yake katika awamu ya kwanza Dkt. Mwinyi amesema ni vyema Viongozi katika Majimbo hayo wakiwemo wabunge wanatakiwa wakachukue madawati hayo ndani ya siku 7 ambapo mwisho itakuwa August 30 2016
Majimbo ambayo hayajachukua madawati yake katika awamu ya kwanza yametajwa kuwa ni Kilindi, Pangani, Makambako, Ludewa, Wangingombe na Makete. Majimbo mengine ni Kyela, Rungwe, Busokelo, Songwe, Kwela, Tunduru, Iringa Mjini, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini na Ileje Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini.
AUDIO. Alichokiongea Waziri Nchemba baada yakufika eneo walipouwawa Askari Polisi Dar


Tukio la kuwawa kwa Askari Polisi wanne katika shambulio lililofanywa na watu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi usiku wa August 23 2016 zimeendelea kuchukua headline ambapo safari hii Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alifika eneo la tukio ambapo pia Ayo TV ilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano.
Waziri Nchemba amesema…>>>’Kumetokea shambulio la uvamizi lenye nia ya uovu ambalo limeua askari wanne, vijana wamefika na wataendelea na msako kuhakikisha waharifu wote wametiwa nguvuni
Tukio lilitokea majira ya saa moja na nusu usiku ambapo bado uchunguzi unaendelea na taarifa kamili itatolewa na Jeshi la Polisi, kifupi ni kwamba shambulio lilifanywa kwa kutumia usafiri wa pikipiki na niwakati vijana wakibadilishana lindo lakini niwahakikishie wananchi kuwa watuhumiwa wote watatiwa hatiani‘ –Waziri Mwigulu Nchemba
AUDIO: Kauli ya msajili wa vyama vya siasa kuhusu wanaotaka kuandamana


Wakati chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kikiwa kwenye mkakati wake wa Operesheni UKUTA (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania) ambao kilele chake kimepangwa kuwa September Mosi mwaka huu ambapo wamepanga kufanyika kwa maandamano nchi nzima.
Leo August 23 2016, msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amekutana na vyombo vya habari na kusema……>>>’Nawasihi wadau wote wenye mipango ya maandamano, mikutano n.k wangesubiri kwanza tuzungumze, ninaamini katika jitihada za kuzungumza hatutakwama kupata ufumbuzi unaostahili au unaotegemewa na wanachi wengi

PICHA 14: Rais Magufuli alivyopokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi wanne


August 23 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka Mabalozi wanne wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi hao ni Roberto Mengoni -Balozi wa Italia hapa nchini, Kim Yong Su – Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea hapa nchini, Mohamed Hassan Abdi – Balozi wa Jamhuri ya Somalia hapa nchini na Paul Sherlock – Balozi wa Ireland hapa nchini.
Akizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati za utambulisho za Mabalozi hao Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itawapa ushirikiano wa kutosha ili kuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano ulipo kati ya nchi hizo na Tanzania.
Dkt. Magufuli amewaambia Mabalozi hao kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 Tanzania imedhamiria kutekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda, hivyo amezialika nchi zao na sekta binafsi katika nchi hizo kuungana na Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na biashara.
Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ireland Paul Sherlock alisema…….>>>Naomba kukuhakikishia kuwa Wafanyabiashara watakaokuja kuwekeza ama kufanya biashara, mitaji yao itakuwa salama na Serikali yangu itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na unanufaisha pande zote mbili” 

Rais Magufuli na balozi wa Italy hapa nchini Roberto Mengoni Ikulu jijini Dar es Salaam.
2
Rais Magufuli na Roberto Mengoni mara baada ya kupokea Hati zake za Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
3
.
4
5
Rais Magufuli na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea hapa nchini Kim Yong Su mara baada ya kupokea Hati zake za Utambulisho
6.
.
6
.
7
Rais Magufuli na Balozi wa Somalia hapa nchini Mohammed Hassan Abdi mara baada ya kuwasili Ikulu kwa ajili ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho.
9
Rais Magufuli na Balozi wa Ireland hapa nchini Paul Sherlock Ikulu jijini Dar es Salaam.
8 10. 11 12. 13

Thursday, 14 July 2016

Tundu Lissu hali tete Kisutu, mahakama yatupilia mbali ombi lake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ya kufutiwa mashitaka ya uchochezi yanayomkabili na wenzake watatu.
Tundu Lissu na wenzake kupitia kwa wanasheria wao waliwasilisha maombi yao katika mahakama hiyo ya kutaka mahakama kufuta mashtaka hayo kwa madai kuwa hati ya mashtaka imekosewa kwani haielezi vya kutosha kuhusu makosa wanayotuhumiwa kuyatenda.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilieza jana kuwa baada ya kupitia hoja za pande zote mbili (mshataki ambaye ni Jamhuri na mshtakiwa ambaye ni Tundu Lissu na wenzake) walijiridhisha kuwa hati hiyo haina makosa.
Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuchapisha habari ya uchochezi kwenye gazeti yenye kichwa cha habari kilichosomeka “Machafuko Zanzibar”. Habari hii ilichapishwa kati ya Januari 12-14 mwaka huuna inadaiwa ililenga kuwatisha wananchi wa Zanzibar wasijitokeze kwenye uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu.
Pamoja na na Tundu Lissu, washtakiwa wengine ni pamoja na mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Sumaye: Nitaing’oa CCM kabla sijaondoka duniani

Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Frederick Sumaye akifurahia fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani ya chama hicho baada ya kukabidhiwa na Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara (kushoto) Dar es Salaam jana.Kulia ni mwanasheria wake, Aidan Kitare.
Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Frederick Sumaye akifurahia fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani ya chama hicho baada ya kukabidhiwa na Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara (kushoto) Dar es Salaam jana.Kulia ni mwanasheria wake, Aidan 

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema ndoto yake ni kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kinang’oka kabla ya kuondoka kwake duniani.
Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitoa kauli hiyo  jana  baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea uenyekiti wa Kanda ya Pwani kwa chama hicho.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyejiunga na Chadema Agosti mwaka jana, alikabidhiwa fomu hiyo na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Mwita Waitara  nyumbani kwake, Kiluvya mkoani Pwani jana.
Alisema sasa ni wakati  wa kukipeleka chama hicho kikuu cha upinzani nchini, hadi vitongojini ambako ndiko wanakojivunia CCM.
”Ndoto yangu ni ile ile iliyonitoa CCM…katika demokrasia kwa mfano Marekani, huwezi kuona wamarekani wamekiacha chama kimoja kitawale miaka 30 hadi 40, hata miaka minane ni bahati sana.
“Nitahakikisha CCM inang’oka madarakani kabla sijaondoka duniani,”alisema.
Aliwashukuru wanachama waliomchukulia fomu kwa kuonyesha imani kwake huku akiahidi kukiimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya chini.
“Nawashukuru kwa kunichangia Sh milioni moja ya kunichukulua fomu, najua mmefanya hivi kwa upendo wenu wala si kwa ubaya nami nasema nimekubali ombi lenu, pia naomba mnipigie kura msiishie hapa,”alisema Sumaye.
Akizungumzia   upinzani kuzuiwa kufanya mikutano, Sumaye alisema kitendo hicho kitaufanya upinzani   uimarike zaidi.
“Kitendo cha kuzuia mikutano ya upinzani si kwamba itaunyong’onyeza bali utaimarika zaidi kwa sababu wananchi wanaona na wanajua kwamba Serikali inawabana wapinzani wasitoe maoni yao  waweze kupimwa kwa maoni hayo.
“Kuminya demokrasia si sahihi… imani yangu watanzania wengi watachukia CCM. Ni nafasi nzuri kwa upinzani kukua na itasaidia upinzani kutoa kura,”alisema.
Awali,   Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, alisema wameamua kumchukulia fomu Sumaye kutokana na uzoefu wa uongozi  alionao  na katika utumishi wa umma.
Waitara ambaye aliongozana na baadhi ya makada wa chama hicho alisema wanamwamini Sumaye kwamba ni kiongozi shupavu atakaye saidia kukijenga chama hicho.

MTANZANIA

Friday, 9 October 2015

NAMNA AMBAVYO WAFANYAKAZI MNAWEZA KUGOMA KISHERIA.


   bashiryakub.blogspot.com
Na  Bashir  Yakub.
MARA  kadhaa  migomo  ya wafanyakazi imekuwa  ikizaa athari  mbaya kwao. Hii  ni  kutokana  na  kugoma  bila  kufuata  taratibu. Waajiri  wao  ni  wajanja. Huwa  makini  sana linapoibuka  wazo  la  kugoma  na  huwa  tayari  muda  woote  kufuatilia  nyendo  ili  panapo  kosa  kidogo  watumie  mwanya  huo  kuwadhibiti   wagomaji.  

Na  kikubwa  wanachofanya hali  ikishakuwa  hivi  ni   kusema  mgomo  haukuwa  halali  na  hapo  kupata  nafasi  ya  kuwashugulikia  waliohusika  katika  kugoma mmoja baada  ya  mwingine.  Katika  mazingira  kama  haya  ni  vema  wafanyakazi  kufahamu  taratibu  za  kisheria  zinazohusu  mgomo  ili  wakati  wa  kufanya  hivyo  asitokee yeyote  kati  yao  wa  kuathiriwa  na  ugomaji  huo.

1.SHERIA  INAMRUHUSU  MFANYAKAZI  KUGOMA.
Wapo  wanaodhani  kugoma  ni  uasi.  Kwa  mfanyakazi  hili  si  kweli.  Kugoma  ni  haki  ya mfanyakazi  kama  zilivyo  haki nyingine.  Kama  ilivyo    haki  ya  kupokea mshahara,  haki  ya kulipwa  muda wa  ziada,  haki  ya muda  maalum  wa  kufanya  kazi, likizo  na  haki  nyinginezo   kwa  ujumla  wake. Kugoma  si  dhambi   isipokuwa  takwa  halali  la  kisheria.  Kitaalam  mgomo  wa  wafanyakazi  huitwa  “strikes” .  Ni  hatua  ambapo  wafanyakazi  hugomea  kuingia  maeneo  ya  kazi  au  huingia  maeneo  ya  kazi  lakini  wasitoe  huduma  kama  ilivyo  ada yao.  

Kisheria  kugoma  ni  jukwaa  la  kuitisha  mjadala  wa  kujadii  maslahi  ya  kazi  kati  ya  mwajiri  na  mwajiriwa.  Kugoma  ni  Jambo  halali  kisheria  ndicho  ninachotaka  kusema  na  kuwatoa  hofu  baadhi  wajuao  kugoma  ni  uasi  na  usaliti.Na haya  ni  kwa mujibu  wa kanuni  namba  ya 42,sheria  namba 6 ya  ajira  na  mahusiano  kazini.

2.  WAFUATAO  HAWARUHUSIWI  KUGOMA.
Makundi  ya  wafanyakazi  watoao  huduma  muhimu  katika  jamii  migomo  kwao  imeharamishwa.  Huduma  muhimu  katika  jamii   hutegemea  na  mahitaji  ya  jamii  husika. Yumkini  hapa  kwetu  huduma muhimu  katika  jamii  hujumuisha watumishi  katika  idara  za  afya, maji  safi  na  salama,  nishati  na  umeme,  vyombo  vya  ulinzi  na  usalama, zimamoto  na  watoa huduma  ya  kuongoza  ndege.  Sababu  kubwa  za  kuzuia  makundi  haya  kugoma  ni  kuwa  kugoma  kwao  huweza kuleteleza  hasara  ambazo  kwazo  haziwezi  kufidiwa  na  kitu  chochote    baada  ya  kutokea kwake.  Na   hasara  kubwa zaidi  hapa  ni  vifo  na  ulemavu  wa  kudumu vitu  ambavyo  haviwezi  kufidiwa  kwa  namna  yoyote na  kitu  chochote .

3.  WANAOTAKA  MGOMO  HALALI  WAFUATE  UTARATIBU  HUU.
( a ) Kwanza  kabisa  hakikisheni  mgomo  wenu  unahusu  maslahi  ya  kazi  yenu.  Usiwe  mgomo  ambao nyuma  yake  wako  watu  hasa  wanasiasa  wanaowasukma  ili  kutimiza  haja  zao fulani. Au  usiwe  mgomo  ambao  umeandaliwa  lengo  likiwa  kumkomoa  mwajiri.  Ni  lazima  kuwepo  na  nukta   muhimu  na  ya  wazi  kabisa  inayohusu  maslahi  katika  kazi  yenu.
( b ) Kabla  ya  kugoma  lazima  muwe  mmepitia  hatua  ya  usuluhishi( mediation). Na  mnapokuwa  mmepitia  hatua hii  ni  lazima  iwe  imethibitika  kuwa  hatua  hiyo  imeshindwa  kutatua  mgogoro  wenu  na  sasa  hatua  inayofuata  ni  ya  kugoma.  Ikiwa  hatua  ya  usuluhishi  imefanikiwa  na kutoa  majawabu    ya  mgogoro  itakuwa ni  haramu  kwa yeyote  kugoma. Kugoma  ni  pale  tu  hatua  ya  usuluhishi  inaposhindwa   na  hatua  hii  hutakiwa  kuchukua  muda  wa  siku  thelathini. Ni  muda  huo utakaotumika  kutafuta  muafaka  kabla  ya  kutangaza  mgomo.
( c ) Ikiwa  mgomo  utakuwa  umeitishwa  na  chama  cha  wafanyakazi  basi kura  za  wengi  ndizo  zitakazotoa  ruhusa  ya  kugoma. Ikiwa  wengi  watakataa  basi  hakuna  mgomo.
( d ) Baada  ya usuluhishi  kushindikana  wafanyakazi  wanaolenga  kugoma  watatakiwa  kutoa  taarifa(notice)   ya  masaa  48  sawa  na  siku  mbili kwa  mwajiri   kabla ya  kuanza  kugoma. Ni baada  ya  muda  huo  ndipo mgomo  utaanza.
( e ) Ikiwa mgomo  utaahirishwa  baada  ya  masaa  48  yaliyokuwa  yametangazwa  kupita,  basi   kama  mnatarajia   kuendelea  na  msimamo  wa  kugoma  mtatakiwa  kutoa  muda mwingine  wa  masaa  48.
Kama  wafanyakazi watafuata  utaratibu  huu  kugoma   hakuna  madhara  yoyote mabaya  yatakayotokea  kwao ikiwa  ni  pamoja  na  kutishiwa  kufukuzwa  kazi.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
RAIS NYUSI WA MSUMBIJI AMWANDALIA JK DHIFA MAALUM YA KUMUAGA, JIJI LA MAPUTO LAMTUNUKU UKAZI WA KUDUMU


 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mwenyeji wake Rais Felipe Jacinto Nyusi  wa Msumbiji wakigonga glasi ya kutakiana heri wakati wa dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais Kikwete na ujumbe wake katika ikulu ya nchi hiyo jijini Maputo maarufu kama Ponta Vermelha usiku wa kuamkia leo.Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuwaaga wananchi wa Msumbiji akisisitiza kuwa uhusiano wa kidugu na kipekee kati ya nchi hizo mbili utaendelea kudumu na kukua
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mwenyeji wake Rais Felipe Jacinto Nyusi wakisimama wakati nyimbo za Taifa zikipigwa wakati wa dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais Kikwete na ujumbe wake katika ikulu ya nchi hiyo maarufu kama Ponta Vermelha usiku wa kuamkia leo.
 Mstahiki Meya wa Jiji la Maputo Mh.David Simango akimvisha Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete vazi maalum na kumkabidhi Ufunguo wa jiji la Maputo kama ishara ya kumtunuku ukazi wa kudumu wa heshima wa jiji hilo wakati wa hafla iliyofanyika katika Jumba la Halmashauri ya jiji la Maputo

 Mstahiki Meya wa Jiji la Maputo Mh.David Simango akijiandaa kumpa  Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete  Ufunguo wa jiji la Maputo kama ishara ya kumtunuku ukazi wa kudumu wa heshima wa jiji hilo wakati wa hafla iliyofanyika katika Jumba la Halmashauri ya jiji la Maputo.
MKUU WA MKOA WA MWANZA KUSHIRIKI ROCK CITY MARATHON

 Katibu wa idara ya utumishi wa waalimu mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani (wa pili kushoto), akipokea fomu ya usajili kutoka kwa Katibu wa chama cha riadha Mwanza, Peter Mujaya (wa pili kulia), kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye jana alijisajili rasmi kushiriki katika mbio za kilomita tano katika mbio za Rock City Marathon zinazotarajia kufanyika tarehe 15 Novemba, 2015 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Wanaoshuhudia ni Kaimu Afisa Michezo mkoa wa Mwanza, Kizito Bahati (kushoto) na Mratibu wa mbio za Rock City Marathon kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bi. Adella Lamsa (kulia).
 Katibu wa idara ya utumishi wa waalimu mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani, akisaini fomu ya usajili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye jana alijisajili rasmi kushiriki katika mbio za kilomita tano katika mbio za Rock City Marathon zinazotarajia kufanyika tarehe 15 Novemba, 2015 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Wanaoshuhudia ni Kaimu Afisa Michezo mkoa wa Mwanza, Kizito Bahati (kushoto) na Katibu wa chama cha riadha Mwanza, Peter Mujaya (kulia).
Na mwandishi wetu
Ikiwa ni siku chache kupita baada ya uzinduzi wa mbio za Rock City Marathon 2015, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. Magesa Mulongo amekua mtu wa kwanza kujisajili kushiriki mbio hizo zilizopangwa kufanyika Novemba 15 mwaka huu katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akizindua usajili wa ushiriki wa mbio hizo jijini Mwanza jana, Mulongo, aliyewakilishwa na Katibu idara ya utumishi wa waalimu mkoa wa Mwanza, Bw. Genzi Sahani, alitoa  wito kwa wanariadha nchini kujitokeza kwa wingi ili kuongeza ushindani wa mbio za mwaka huu, ambazo zimekuwa na lengo la kuhimiza utalii wa ndani nchini.

 “Nimekuwa mfuatiliaji wa mbio hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 2009 na tumeshuhudia viwango vya mbio hizi vikipanda kila mwaka, kitu ambacho ni kielelezo cha kuonyesha maandalizi mazuri yanayofanywa kwa kuzingatia viwango na sheria zilizo wekwa,” alisema Mulongo katika shughuli hiyo iliyohudhuliwa na wadau mbalimbali wa mchezo wa riadha.

Mulongo, alisema kuwa katika miaka ya hivi karibuni mchezo wa riadha umekua ukififia na kutaka wadau mbalimbali, ikiwemo makampuni binafsi, kuunganisha nguvu ili kuurudisha kwenye ramani mchezo huo ulioliletea taifa sifa kubwa katika miaka ya nyuma.

“Ni kweli kwamba makampuni na hata watu binafsi wanajitokeza kusaidia kukuza mchezo wa riadha hapa nchini, lakini bado mchezo huu una changamoto nyingi hususani katika mkoa wetu wa Mwanza na bado zinahitajika jitihada za ziada kwa wadau mbali mbali wa mchezo huu kushirikiana ikiwa ni pamoja na makampuni binafsi bila kusahau viongozi wa chama cha Riadha Mkoani Mwanza,” alisema.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Meneja wa Shirika la hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Mwanza Shaaban Luanda, ambao ni wadhamini wakuu, alisema: “Mbio za Rock City Marathon zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua mchezo wa riadha nchini. Sisi kama shirika la hifadhi ya jamii tunaamini kupitia michezo tunaweza kulinda afya ya jamii na ndio maana tumeendelea kudhamini mbio hizi.