Bahati lusambo: Local News

Sunday, 28 August 2016

Profesa Lupumba,Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya Wavuliwa Uanachama CUF

Chama Cha Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya.

Uamuzi huo umetolewa jana na Baraza Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake visiwani Zanzibar kwa lengo la kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kabla ya kusimamishwa.

Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua.

Mbali na vigogo hao, wengine waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee, Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya.

Aidha, Baraza hilo limemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. Hatua hii inaweka matatani ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Lipumba na Sakaya hawakupata nafasi ya kujitetea kutokana na kutohudhuria mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi ya kujitetea kutokana na uwepo wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda. Katiba ya chama hicho haiwapi nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Baraza hilo.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku chacha baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliolenga kumchagua Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo vurugu kubwa baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na wafuasi wake wakitaka barua yake ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake ijadiliwe na kukubaliwa.

Hata hivyo, kura zilizopigwa na wajumbe wote zaidi ya 800, ni kura 14 pekee zilizotaka Profesa Lipumba aendelee na nafasi ya uenyekiti.
Askari Magereza Atiwa Mbaroni Kwa Kuingia Wodini Akiwa Amelewa na Kisha Kuanza Kufyatua Risasi


POLISI mkoani Rukwa inamshikilia askari Magereza, Cleophas Chapaulinge kwa kosa la kulewa na kupiga risasi hewani akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga na kusababisha taharuki kubwa kwa wagonjwa na wauguzi.

Kitendo cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba tisa ya wanawake na watoto, ambapo akinamama walipiga mayowe kwa hofu huku wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha watoto wao vitandani.

Akizungumza  kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha kutokea kwa tukio hilo  na kueleza kuwa lilitokea jana alfajiri.

“Chanzo ni ulevi wa kupindukia tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha kipimo ni alama kati ya 70 na 40 …. Katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10,” alisema.

Kamanda Kyando alisema siku ya tukio, askari huyo akiwa na mwenzake walikuwa kwenye lindo akilinda makazi ya Kamanda wa Magereza wa Mkoa, lakini alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba tisa, ambako mkewe alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.

Mke wa mtuhumiwa huyo, Theresia Kalonga ambaye naye ni askari Magereza, alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.

“Mtuhumiwa huyo tunamshikilia huku taratibu za kumkabidhi kwa Kamanda wa Magereza Mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea,” alisisitiza Kamanda Kyando.

Akizungumza hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha alisema askari huyo baada ya kuingia wodini, aliweka silaha yake chini akafunua chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje na kufyatua risasi hewani na kutoboa paa.

“Mtuhumiwa huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa,” alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa hospitalini hapo na mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa, lakini alisababisha taharuki kubwa hospitalini.

“Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwahi kufika hospitalini hapo na kumtia nguvuni, na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa ikiwa na risasi kumi,” alisema.

Muuguzi wa zamu wodini humo, Rose Katabi alisema askari huyo alipofyatua risasi akinamama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha muuguzi kwa ajili ya kusalimisha maisha yao.

“Kwanza kitendo cha kumuona askari huyo akiwa na silaha mkononi, mwili wangu wote ulikufa ganzi nilihisi atatulipua kwa kutupiga risasi za moto …aliiweka silaha yake hiyo chini na kuanza kuzungumza na mwanawe. Aliniuliza kama mtoto wake ameshakunywa dawa, nikamjibu anakunywa dawa mara moja usiku.

“Waliingia walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza, kusema atarudi tena, akatoka nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua risasi hewani iliyotoboa paa kisha akaondoka na kutokomea gizani,” alisema.

Kwa upande wa mke wa mshtakiwa huyo, Theresia alisema alipomuona na sare za jeshi na silaha mkononi alimtaka arudi mara moja kazini. 
Walinzi waliokuwa kwenye lindo katika lango kuu la kuingia hospitalini hapo kwa masharti ya kutoandikwa majina yao , walidai kuwa askari huyo alifikishwa hospitalini hapo kwa usafiri wa bodaboda.

“Alitutia shaka baada ya kukataa kusimama, kwani alipitiliza moja kwa moja akiwa na silaha mkononi, tulijawa na hofu kubwa tukaamua kumfuata kwa nyuma hadi akaingia wodi namba tisa alikolazwa mkewe na mtoto wake. Lakini tulipomuona akikoki bunduki yake tulilazimika kukimbia na kwenda kujificha ndipo tukasikia mlio wa risasi,” alisema mmoja wao.
Godbless Lema Agoma Kula Kwa Saa 48


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ( Chadema) anayeshikiliwa katika mahabusu ya kituo kikuu cha Arusha Mjini amegoma kula kwa zaidi ya saa 48 sasa tangu alipokamatwa

Lema alikamatwa juzi alfajiri akiwa nyumbani kwake Njiro Arusha kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi  na kushawishi watu kwa njia ya mtandao waandamane Septemba mosi.

Jana Meya wa Arusha, Calist Bukhay alisema Lema amegoma kula

Alisema Lema aligoma kula akidai kuwa alifanyiwa udhalilishaji mbele ya watoto wake wakati polisi walipokuwa wakitekeleza agizo la kumkamata.

"Ni kweli amegoma kula tangu jana (juzi) alipokamatwa.Alisema askari polisi walipkwenda kumkamata walimfanyia vitendo vya udhalilishaji mbele ya watoto wake na kumnyanyasa bila kujali yeye ni kiongozi wa wananchi.

"Sasa  yeye ameshikilia msimamo wake kuwa kwa kuwa polisi walikuwa wamepanga kumuua wakati wa kumkamata, basi ni bora akafa kwa njaa.

"Chakula kimekuwa kikipikwa na kupelekwa na mkewe ,lakini bado amegoma kukila.Baada ya tukio hilo, polisi walituita ili kujaribu kumshawishi ale mchana, akagoma" Alisema Meya Calist.

Thursday, 25 August 2016

Mtoto aliyepotea akutwa chooni akiwa amefariki,huku akiwa na jamaa wa jirani



Huzuni imetanda katika mtaa mmoja wa Tabata jijini Dar es salaam baada ya mtoto wa miaka 3 kufariki katika mazingira ya kutatanisha.Mtoto huyo ambaye ni wakiume alipotea  na baada ya kutafutwa  sanaa alikuja kupatikana chooni akiwa na jamaa mmoja huku mtoto akiwa hana nguo.
Wananchi walianza kumshushia kipondo jamaa huyo mkatili kabla ya kumpeleka polisi huku mtoto akikimbizwa hospitali bila kujua kwamba tayari alikuwa ameshafariki.

Uchunguzi wa daktrai ulionyesha kuwa hakuna kitu chochote kibaya ambacho mtoto alichofanyiwa lakini inasemekana njemba hilo lilimkaba mtoto ili asipige kelele.
Huzuni imetanda mtaani hapo huku wazazi wakiwa nahofu kubwa kwa watoto wao hata kuwaruhusu kwenda nje kucheza wanaogopa.Kinachoumiza zaidi ni kwakuwa jamaa huyo ni wa hapohapo mtaani na watu wanamjua.


CHADEMA Wapinga Kauli ya Jeshi la Polisi Kuzuia Mikutano ya Ndani ya Vyama vya Siasa

Wakati Jeshi la Polisi likisisitiza kupiga marufuku mikutano na maandamano ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (Ukuta), chama hicho kimepinga katazo hilo nakudai kuwa ni haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao Makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, jijini Dar es Salaam.

Kwenye mkutano huo akiwa na Lawrance Masha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani (2005-2010) Lissu amesema, rais anayo nafasi ya kuzuia mikutano ya hadhara kwa sharti la kupeleka hoja bungeni na kisha kujadiliwa na si vinginevyo.

“Ipo sheria ya kutangaza hali ya dharura, iliyotungwa mwaka 1995, hii inamruhusu rais kupeleka hoja bungeni ya kutaka kutangaza hali ya dharura kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu na kama Bunge likiridhia, basi rais anatangaza, namshauri Magufuli afanye hivyo.

“Aitangazie Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa, nchi hii ipo katika hali ya hatari na katika hali ya dharura, na kwamba mikutano yote itakuwa marufuku.

“Na miezi mitatu ikiisha aende tena bungeni kuomba aongeze mingine. Akifanya hivyo atakuwa hajavunja sheria na hata sisi tutamtii,” amesema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutoa matamko yanayoiingiza nchi katika utawala wa kidikteta.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tu, tangu jeshi hilo kupitia Nsato Marijani, Kamishina wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, litangaze kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa nchini, ikiwemo vikao vya ndani vya vyama.

Katika mkutano na wanahabari, makao makuu ya chama hicho, akiwa ameambatana na Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu, pamoja na Masha amesema, Lissu amesema, kamwe Chadema hakiwezi kuruhusu ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.

“Amri ya jana ya polisi, wakipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa ikiwemo vikao vya ndani ni muendelezo wa amri haramu na kitendo hicho cha jana na vingine vilivyopita, ni mfano hai ya kwamba, nchi yetu imeingia katika mfumo wa udikteta.

"Kwani, kwa mujibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967; udikteta ni utawala wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache wanaofikiria kwamba, amri zao ndiyo sheria na wote wanaowapinga, hukiona cha mtema kuni,” amesema Lissu.

Lissu amesema kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya sasa pamoja na sheria zote ikiwemo Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, Sheria ya Maadili ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2007 pia sheria za Jeshi la Polisi, hakuna mahali ambapo polisi au rais anaruhusiwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.

“Anayetakiwa kujulishwa kuhusu uwepo wa maandamano na mikutano ya hadhara ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na kama kuna tatizo kwa muda huo, anaweza kuelekeza isifanyike kwa muda fulani lakini siyo Rais Magufuli wala Nsato,” amesema.

Wakati Lissu akisema hayo, Masha amesema, “nimekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miaka mitano, lakini sikuwahi kupiga marufuku mikutano ya hadhara wala ile ya ndani. Nilifahamu kuwa, kuna umuhimu wa watu kuzungumza, kukosoana na kuelimishana.

"Ni vyema Rais Magufuli akajua, hii ni nchi ya kidemokrasia na kuna Katiba na sheria ambazo kila mtu ni lazima afuate akiwemo yeye, matamko ya kibabe ya Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la polisi ni kinyume na sheria pamoja na Katiba yetu.”

Dk. Mashinji, amesisitiza kuwa, Chadema kipo tayari kwa mazungumzo na mamlaka yoyote ya serikali juu ya azma ya kufanya mikutano na maandamano, ili mradi tu sheria na katiba ya nchi izingatiwe katika mazungumzo hayo.

“Hatujafunga milango ya mazungumzo na serikali, tunachosisitiza sisi ni kuwa hata kama kuna mazungumzo yatafanyika, Katiba na sheria za nchi yetu lazima zizingatiwe,” amesema Dk. Mashinji.

Wednesday, 24 August 2016

Jeshi La Polisi Lahusisha Mauaji ya Polisi Wanne na Sakata la Oparesheni UKUTA.........Lapiga Marufuku Mikutano yote ya Ndani ya Vyama vya Siasa
KUFUATIA mauaji ya askari wanne yaliyotokea Kata ya Mbande Temeke kwa watu wanaodhaniwa ni majambazi kuvamia benki ya CRDB na kuwaua askari hao kwa kutumia silaha za moto jeshi la Polisi limetangaza kiama na kuwataka wahusika wote kujisalimisha.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi limehusisha tukio hilo na Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) kufuatia matamko ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha wafuasi wao wawashambulie askari wa Jeshi la Polisi.

Kauli hiyo imetolewa  na Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Nsato Marijan Mssanzya (CP), wakati akizungumza waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana ambapo pia alikiri kuwa mazoezi yanayofanywa na polisi yamelenga kukabiliana na Ukuta.

Akizungumza kwa hisia CP Mssanzya pia amepiga marufuku  mikutano ya ndani yenye viashiria vya uchochezi na hata ikifanyika kwenye majukwaa watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa sheria.

Amesema Jeshi  hilo limebaini kwamba mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuchochea wananchi na kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi na kufanya mapambano na jeshi la polisi

"Kwasababu hiyo basi,kwa hali ya kutumia mikutano ya ndani kuchochea watu kuvunja sheria na kupambana na askari, hivyo basi kuanzia sasa jeshi la polisi nchini linapiga marufuku mikutano yote ya ndani" amesema.
 
Aidha CP  Mssanzya  aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo wakati wakibadilishana lindo kuwa ni  E.5761 CPL Yahya, F.4660 CPL Hatibu, G 9524 PC Tito na G 9996 PC Gastoni na raia wawili waliojeruhiwa aliowataja kuwa Ali Chiponda na Azizi Yahya wote wakiwa wakazi wa Mbande.

"Katika tukio hilo majambazi ambao idadi yao haikufahamika walifanikiwa kupora silaha mbili aina ya MSG na lisasi 60 na hakuna pesa wala mali ya benki hiyo kuibiwa au kuharibiwa, ni dhahiri kuwa waharifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambiulia askari polisi, " alisema.

Alisema katika hali ya kushangaza baada ya tukio hilo kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukeji mazoezi ya kawaida ya jeshi la polisi na wengine waliandika ujembe wa kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari polisi huku wengine wakidiriki kuandika ujumbe unaosema endapo watapigwa na polisi Septemba1 mwaka huu basi viongozi wa jeshi hilo wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi limejipanga vyema kukabiliana na matukio yote ya uvunjifu wa amani nchini.
Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.