Sunday, 28 August 2016

Profesa Lupumba,Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya Wavuliwa Uanachama CUF

Chama Cha Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya.

Uamuzi huo umetolewa jana na Baraza Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake visiwani Zanzibar kwa lengo la kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kabla ya kusimamishwa.

Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua.

Mbali na vigogo hao, wengine waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee, Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya.

Aidha, Baraza hilo limemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. Hatua hii inaweka matatani ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Lipumba na Sakaya hawakupata nafasi ya kujitetea kutokana na kutohudhuria mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi ya kujitetea kutokana na uwepo wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda. Katiba ya chama hicho haiwapi nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Baraza hilo.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku chacha baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliolenga kumchagua Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo vurugu kubwa baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na wafuasi wake wakitaka barua yake ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake ijadiliwe na kukubaliwa.

Hata hivyo, kura zilizopigwa na wajumbe wote zaidi ya 800, ni kura 14 pekee zilizotaka Profesa Lipumba aendelee na nafasi ya uenyekiti.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: