Aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi nchini Zimbabwe Jenerali Constantino Chiwenga ambaye aliongoza mapinduzi baridi ya kijeshi dhidi ya Robert Mugabe anatazamiwa kuapishwa leo Alkhamisi kuwa makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo.
Chiwenga ataapishwa pamoja na mwanasiasa mkongwe nchini humo, Kembo Mohadi kuwa makamu mwenza wa rais katika Ikulu ya Harare.
Jumamosi iliyopita, Rais Mnangagwa aliwateua wawili hao kuwa manaibu wake ndani ya chama tawala Zanu-PF. Hii ni licha ya viongozi wa upinzani na wakosoaji wa serikali kupinga uteuzi wa wawili hao na hata ule wa mawaziri, wakisema kuwa aghalabu ya walioteuliwa na Mnangawa walihudumu ndani ya utawala wa Mugabe.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Msemaji wa Rais wa Zimbabwe, George Charamba alisema uteuzi wa wawili hao kuwa makamu wa rais wa nchi ungeweza kufanywa tu na Katibu Mkuu wa serikali na baraza la mawaziri, Misheck Sibanda ambaye wakati huo alikuwa nje ya nchi.
Mnangagwa aliapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe tarehe 24 Novemba, siku tatu baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe kutangaza kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya kila upande.
Rais huyo mpya wa Zimbabwe anakabiliwa na mashinikizo ya ndani ya nje ya nchi ya kutekeleza mageuzi ya kisiasa aliyoahidi mara baada ya kula kiapo zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
0 comments: