WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya
kuvunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili ambao
ndiyo chanzo pekee cha maji cha Wilayani Nkasi atatozwa faini ya sh.
milioni 70 pamoja na kifungo miaka saba jela.
Katika
kuhakikisha hatua zinachukuliwa Waziri Mkuu amemkabidhi mkuu wa wilaya
ya Nkasi, Said Mtanda kitabu cha sheria kitachomuangoza katika
kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya uharibifu katika
chanzo hicho cha maji.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati
akizungumza na wananchi wa mji Mdogo wa Namanyere katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye viwanya vya Sabasaba.
“Mkuu
wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua za kuwaondoa wananchi na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliovamia maeneo ya
hifadhi za misitu na kuanzisha makazi au kufanya shughuli za kijamii
naye atakuwa jipu,” alisema.
Waziri
Mkuu alisisitiza kuwa maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya
upatikanaji wa maji baada ya wananchi kuvamia katika vyanzo vya maji na
kufanya shughuli za kibinadamu hivyo kusababisha vyanzo vingi kukakuka
“Serikali
haitakubali kuona mtu anaharibu chanzo cha maji. Wananchi mnatakiwa
kuwa walinzi wa maeneo hayo na atakayekutwa anachunga mifugo, analima,
kukata nyasi au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya maeneo hayo
atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Awali
Waziri Mkuu alikagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji Mfili ambalo
mwanzo lilikuwa na ujazo wa lita 1,500 ambapo litakapokamilika litakuwa
na ujazo wa lija 248,067 hivyo kuwezesha wakazi 82,689 kunufaika.
Akizungumza
kwenye eneo la mradi mara baada ya Waziri Mkuu kuwasili, Mkurugenzi
Mtendaji wa wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo alisema hadi kukamilika mradi
huo unatarajiwa kugharimu sh trilioni 1.011 ambapo Wizara ya Maji na
Umwagiliaji imetoa sh. milioni 500 na OOfisi ya Rais TAMISEMI itatoa sh.
milioni 500.
Mkurugenzi
huyo alisema mradi unakabiliwa na changamoto ya ukosefu umeme ppamoja
na mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya umeme, ambapo
aliiomba Serikali kuipatia halmashauri hiyo sh. milioni 222.576 ikiwa ni
gharama za kupeleka umeme kwenye eneo la mradi na kununua mitambo.
Mbali
na kutembelea mradi wa upanuzi wa bwawa, pia Waziri Mkuu alitembelea
hospitali teule ya wilaya ya Nkasi na kuzindua wodi mpya yenye uwezo wa
kulaza wagonjwa 72 kwa wakati mmoja
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, JUMATANO, AGOSTI 24, 2016.
Safi
ReplyDelete