Mvutano
kuhusu maelezo ya mlalamikaji katika kesi ya uchochezi inayomkabili
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, baina ya mawakili wa upande wa
mashtaka na upande wa utetezi ulikwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika
kesi hiyo Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na
Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa
kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Anadaiwa
kuwa Juni 28, mwaka huu, Lissu akiwa katika viwanja vya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa:
“Mamlaka
ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila
Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila
sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani
ya giza nene.’’
Kesi
hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa leo kwa upande wa mashtaka kuanza
kutoa ushahidi.Wakili wa Serikali Bernard Kongola aliieleza mahakama
kuwa walikuwa na mashahidi wawili ambao aliwataja kuwa ni Mrakibu
Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Staff Sajenti Ndege.
Hata
hivyo kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, kiongozi wa jopo la mawakili wa
Lissu, Peter Kibatala aliiomba mahakama wapewe maelezo ya mlalamikaji
katika kesi hiyo kabla ya kufanya jambo lolote, jambo ambalo liliibua
mvutano wa hoja baada ya kupingwa na upande wa mashtaka.
Wakili
Kongola aliieleza mahakama kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, si miongoni mwa
mashahidi wao wanaokusudia kuwaita mahakamani.
Pia alisema kuwa kwa mujibu wa sheria hawalazimiki kutoa maelezo hayo ya mlalamikaji kwa mtu ambaye si shahidi.
Akijibu
hoja hizo, Wakili Kibatala alidai kuwa taarifa ya huyo mlalamikaji ndio
chanzo au iliyosababisha kesi hiyo na kwamba iwapo watamleta au
hawatamleta lakini maelezo yake ni sehemu ya kesi hiyo.
Alidai
kuwa hata mashtaka yaliyopo chini ya sheria ya magazeti ni ya muhimu na
kwamba hawawezi kujitetea bila kuyaona na kwamba hata kama upande wa
mashtaka hautamuita, wao wataiomba mahakama aitwe kwa lazima.
Hivyo aliiomba mahakama iulazimishe upande wa mashtaka uwapatie maelezo hayo ya mlalamikaji.
0 comments: