Thursday, 17 March 2016

Miss Tanzania kuanza tena Machi 19 mwaka huu


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2016  yatakayofanyika Machi 19, 2016 jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mashindano hayo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited kampuni inayoandaa  mashindano hayo Bw. Hashim Lundenga amesema kuwa uzinduzi huo kwa mwaka 2016 utakuwa wa aina yake tofauti na miaka iliyopita.

“Tunatarajia kutangaza kamati mpya ya Miss Tanzania siku hiyo ya uzinduzi, kamati ya Miss Tanzania itakuwa na jukumu la kuusaidia uongozi wa Miss Tanzania katika shughuli nzima za kuratibu na kusimamia mashindano hayo.” alisema Lundenga.

Lundenga ameongeza kuwa, katika uzinduzi huo wadau mbalimbali wa tasnia ya urembo wakiwemo wabunifu wa mavazi, mawakala wanaoandaa mashindano ya Miss Tanzania katika ngazi mbalimbali hapa nchini watakutana .

Aidha  amesema uzinduzi wa Miss Tanzania mwaka 2016 umedhaminiwa na makampuni ya Ramada Resorts Dar, Naf Beach Hotel Mtwara, Kitwe General Trader, CXC Africa, MMI Tanzania, Mwandago Invesment Ltd, Break Point na GSM Media.

Vilevile uzinduzi huo utahamia mkoa wa Arusha mara tu baada ya kufanyika  mkoa wa Dar es Salaam. Wasanii Linah Sanga anayeimba nyimbo za kizazi kipya na Wanne Star msanii wa ngoma za asili watatoa burudani katika uzinduzi huo.

Mashindano ya Miss Tanzania yalifungiwa kwa miaka miwili mfululizo na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Desemba 22, 2014 kutokana na kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, kutokuwasilisha nyaraka mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya washiriki pamoja na kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.

Mashindano hayo yamefunguliwa tena na BASATA Agosti, 2015 baada ya mwandaaji wake LINO International Agency Limited kufuata taratibu ikiwemo kuomba radhi  na kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza pamoja na kutekeleza masharti aliyopewa.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: