Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitoa kauli hiyo jana baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea uenyekiti wa Kanda ya Pwani kwa chama hicho.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyejiunga na Chadema Agosti mwaka jana, alikabidhiwa fomu hiyo na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Mwita Waitara nyumbani kwake, Kiluvya mkoani Pwani jana.
Alisema sasa ni wakati wa kukipeleka chama hicho kikuu cha upinzani nchini, hadi vitongojini ambako ndiko wanakojivunia CCM.
”Ndoto yangu ni ile ile iliyonitoa CCM…katika demokrasia kwa mfano Marekani, huwezi kuona wamarekani wamekiacha chama kimoja kitawale miaka 30 hadi 40, hata miaka minane ni bahati sana.
“Nitahakikisha CCM inang’oka madarakani kabla sijaondoka duniani,”alisema.
Aliwashukuru wanachama waliomchukulia fomu kwa kuonyesha imani kwake huku akiahidi kukiimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya chini.
“Nawashukuru kwa kunichangia Sh milioni moja ya kunichukulua fomu, najua mmefanya hivi kwa upendo wenu wala si kwa ubaya nami nasema nimekubali ombi lenu, pia naomba mnipigie kura msiishie hapa,”alisema Sumaye.
Akizungumzia upinzani kuzuiwa kufanya mikutano, Sumaye alisema kitendo hicho kitaufanya upinzani uimarike zaidi.
“Kitendo cha kuzuia mikutano ya upinzani si kwamba itaunyong’onyeza bali utaimarika zaidi kwa sababu wananchi wanaona na wanajua kwamba Serikali inawabana wapinzani wasitoe maoni yao waweze kupimwa kwa maoni hayo.
“Kuminya demokrasia si sahihi… imani yangu watanzania wengi watachukia CCM. Ni nafasi nzuri kwa upinzani kukua na itasaidia upinzani kutoa kura,”alisema.
Awali, Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, alisema wameamua kumchukulia fomu Sumaye kutokana na uzoefu wa uongozi alionao na katika utumishi wa umma.
Waitara ambaye aliongozana na baadhi ya makada wa chama hicho alisema wanamwamini Sumaye kwamba ni kiongozi shupavu atakaye saidia kukijenga chama hicho.
MTANZANIA
0 comments: