Thursday, 15 May 2014

HOFU YATANDA KIJANA ALIYEUA WAZAZI WAKE

Na Mwandishi Wetu, Moshi
BAADA ya wanadoa wawili, Shahidu Njau (60) na mkewe Minae Swai (57) kudaiwa kuuawa kinyama na Yusuf Njau (32),  anayeaminika kuwa ni mtoto wao, kwa  kuwacharanga kwa shoka Ijumaa iliyopita, hofu imetanda kijijini Masama Rao, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro yalipotokea mauaji hayo.

Yusuf Njau anayedaiwa kuuwa wazazi wake kwa shoka
Hofu hiyo imewakumba baadhi ya wazazi kijijini hapo ambao walidai kuwa, wana wasiwasi mkubwa na vijana ambao wamekuwa na tabia ya kukaa vijiweni wakivuta bangi.
Wananchi hao walioomba majina yao kuhifadhiwa kwa sababu za kiusalama, walisema hayo kufuatia Njau kudaiwa kuwakata shoka wazazi wake kisha kuchoma moto nyumba  yao baada ya kuibuka ugomvi wa kifamilia na kutokomea kusikojulikana kabla ya kumatwa juzi na jeshi la polisi.
Wananchi hao wameliomba jeshi la polisi kuendesha msako kijijini hapo ili kuwanasa vijana wote wanaovuta bangi na kunywa pombe haramu ya gongo kwani wamekuwa tishio kwa maisha ya raia wema.
Maiti zikisaliwa tayali kwa ajili ya mazishi
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Halfani Swai aliungana na wananchi kuomba usalama katika kijiji chao na kuhusu tukio hilo alifafanua kuwa: “Tulikuta mwili wa baba ukiwa pembeni, ukiwa umejeruhiwa vibaya kichwani, ubongo ulikuwa pembeni, tulimchukua kumpeleka hospitali lakini tulipofika kwa Sadala alipoteza maisha,” alisema Swai.
Mwenyekiti Swai alisema kuwa kijana huyo ambaye ni mkorofi sana aliwahi kutishia kuwaua shangazi na baba mdogo wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na akasema atachunguzwa akili yake kabla ya kufikishwa mahakamani.
Maiti zikipelekwa makabulini kwa ajili ya mazishi
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga  (pichani) alisema tukio hilo ni la kinyama na amewataka wananchi kuwa na subira huku akitahadharisha raia kutochukua sheria mikononi.
Marehemu walizikwa siku ya pili yake baada ya kuuawa, kwenye makaburi ya nyumbani, kijijini Masama Roo.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: