JASIRI ALIYESHINDWA KUKABILI CHANGAMOTO ZA NDOA
Na Zuhura Simba
Mwanasiasa Mkongwe na Mwanaharakati
aliyepambana na sera za ubaguzi za makaburu wa Afrika Kusini na hatimaye
kuwa Rais wa kwanza Mwafrika nchini humo. Ni mshindi wa Tuzo ya Amani
ya Nobel. Pia amepata kutunukiwa zaidi ya tuzo 250 katika miongo minne
iliyopita.
Ni Rais wa kwanza aliyechaguliwa
kidemokrasia nchini Afrika Kusini. Alikuwa mwanasheria na mwanachama wa
Chama cha African National Congress (ANC) aliyepinga utawala wa ubaguzi
wa rangi Afrika Kusini.
Pamoja na ushujaa huo wa Nelson
Mandela,katika Maisha yake ya Ndoa alipata changamoto nyingi sana ambazo
alijitahidi kuzikabili bila mafanikio.
Wengi tunajua jinsi ndoa ilivyo na
changamoto kubwa. Wengine wana mawazo kwamba Mungu, hakupanga taasisi
hii (ndoa) iwe ilivyo sasa, ya mme mmoja na mke mmoja au hata kufunga
ndoa; kwamba alituumba tuishi kama wanyama! Bila kuwa na kifungo cha
ndoa!
Haya yanasemwa baada ya ndoa nyingi
kukumbwa na changamoto. Mahatma Gandhi, alifikia hatua ya kutaka kuishi
na mke wake, kama mtu na dada yake.
Walifanya kiapo cha kuacha uhusiano wa
kimwili – uhusiano wa ndoa, ili waishi kama ndugu. Alikuwa tofauti na
Mandela kwani yeye hakuvunja ndoa yake bali aliishi na mkewe kama mtu na
dada yake.
Hali ilikuwa tofauti kidogo kwa upande
wa Nelson Mandela kwa kutoweza kuishi na Winnie kama mtu na dada yake
hii ndo imepelekea leo hii awe ni shujaa lakini alishindwa kustahimili
changamoto za ndoa. .
Hakuna asiyejua ni jinsi gani Madiba
alivyoshinda mitihani mingi kwenye maisha yake lakini kama ilivyo ada
hakuna mkamilifu kwenye dunia hii.
Pamoja na heshima zote tunazompatia Mzee Mandela, alibaki ni mwanamume wa kiafrika mwenye kuutukuza mfumo dume.
Katika vitabu vya historia ya
Mandela,kuna baadhi ya vitabu vilivyomuonesha akimfanyia unyanyasaji wa
kijinsia mkwewe wa kwanza Evelyn,kiasi cha kuwaleta wapenzi wengine
kwenye kitanda chao cha ndoa na kumlazimisha Evelyn kulala uvunguni mwa
kitanda.
Pia Mzee Mandela, hakutaka Winnie afanye
kazi yoyote, alimtaka akae nyumbani na kuwalea watoto. Ukisoma barua
ambazo Mandela alikuwa akimwandikia Winnie, kipindi ambacho alikuwa
gerezani utaona alivyokuwa akisisitiza kuwa mkewe akae nyumbani ili alee
watoto na yeye ndo atakeyehakikisha mahitaji yote kama kichwa cha
familia.
Hii hali haikuwa kwa Winnie peke yake
hata kwa mke wake wa kwanza Evelyn naye alipata changamoto ya kutekeleza
mapenzi ya Mandela kwa jinsi atavyotaka Mandela kama mume na baba
mwenye nyumba.
Evelyn,alikuwa Mkristu mwenye itikadi
kali,ilikuwa vigumu sana kukubali kuchanganya suala la siasa na
hakukubali kuchanganya dini na siasa. Na hakukubali kutekeleza mapenzi
ya baba mwenye nyumba. Hata hivyo, kinyume cha ndoa ya Winnie, kwa
Evelyn, aliyeshinikiza ndoa hiyo kuvunjika si Mandela.
Evelyn mwenyewe ndiye aliweka masharti
ya ama Mandela kumchagua yeye au kuichagua siasa na Mandela, akaamua
kuichangua siasa na ndoa yao ikavunjika.
Mbali na tatizo hili la mfumo dume la
mwanamke kutekeleza mapenzi ya baba mwenye nyumba, mfumo ambao
umezivuruga ndoa nyingi za kiafrika au kusababisha wanawake wengi wa
kiafrika kuishi maisha magumu kwenye ndoa zao, Mzee Mandela alikuwa na
tatizo la kutopata nafasi ya kutosha kusoma na kuelewa tabia za wapenzi
wake.
Alikuwa akivutiwa na sura, muda mfupi
anatangaza ndoa. Ilitokea kwa Evelyn, ikatokea kwa Winnie na hata kwa
mkewe wa mwisho, Graca.
Kwenye kitabu chake cha Long Walk To Freedom,
ukurasa wa 101 anasema; “Siku chache baada ya kukutana na Evelyn, kwa
mara ya kwanza, niliomba kumtoa. Haraka haraka tulianza mapenzi na miezi
michache baadaye niliomba tufunge ndoa, akakubali..”. Pia anaelezea
jinsi Evelyn alivyokuwa msichana mzuri na wa kuvutia.”
Na ukurasa wa 214, Mandela anaandika:
“Siamini kama kuna mapenzi ya papo kwa hapo, lakini nilipokutana na
Winnie Nomzamo, kwa mara ya kwanza, niliamini nataka awe mke wangu..”
Na ndivyo ilivyokuwa, walifunga ndoa na
Winnie, muda mfupi baada ya kukutana. Na historia iliyofuata,
haikumpatia nafasi Mandela, kumfahamu Winnie. Harakati za kupigania
uhuru na hatimaye kifungo cha miaka 27, ulikuwa ukuta mkubwa kati ya
Winnie na Mandela.
Baadhi ya vyombo vya habari vilieleza
jinsi uhusiano wa Graca Marchel na Mzee Mandela ulivyoanza. Mara ya
kwanza alipokutana na mama huyu, Mzee Mandela aliuliza wasaidizi wake “
Huyu Mama mzuri hivi ni nani?”
Wakamjibu ni “Mke wa marehemu Samora
Marchel”. Alipokutana na Graca, mara pili, Mzee Mandela, hakukumbuka
alishatambulishwa, aliuliza swali lile lile “Huyu Mama mzuri hivi ni
nani?” Akajibiwa tena ni “Mke wa Marehemu Samora Marchel”.
Ilipotokea mara ya tatu akaamua kutupa
karata ya kufunga ndoa. Yawezekana kwa ndoa hii ya tatu, Mzee Mandela,
amepata nafasi ya kuangalia mbali zaidi ya sura. Wake zake wawili wa
mwanzo Evelyn na Winnie, alitamani sura zao na kuwataka wayatimize
“mapenzi yake”, hakupata nafasi ya kuangalia na kujifunza kwa undani
karama zao na kuziachia karama hizo kuchanua.
Mzee Mandela, alivutiwa na sura, lakini
hakuwa tayari kuyapokea na yale ya ndani. Evelyn, alipotoa ya ndani, na
kuonyesha kwamba yeye si sura tu bali ana mengine yanayounda “utu”
wake na upekee wa yeye kuitwa ni fulani, Mzee Mandela hakuwa tayari
kuyapokea na ndoa yao ikaishia hapo.
Vile vile kwa Winnie, Mzee Mandela
alivutiwa na sura yake, lakini hakuwa tayari kupokea yale ya ndani.
Winnie, mpambanaji, Winnie mwanasiasa, kwa vile kwa kipindi kirefu
hawakuishi pamoja kuweza kufahamu mambo ya ndani ya Winnie, alipotoka
gerezani na kupata nafasi ya kumfahamu Winnie alivyo, Mzee Mandela,
alishindwa kabisa kumpokea jinsi alivyo. Winnie, mwenye sura nzuri ya
kuvutia, alikuwa sasa ni Winnie mwanasiasa na Winnie mpambanaji. Mzee
Mandela, akafunga milango ya moyo wake na kuanza mbio nyingine za
kumtafuta mwenza mwingine.
Ndoa, ni kuunganisha watu wawili
wasiofanana! Watu wawili ambao si ndugu wala jamaa! Ndoa ni
kuunganisha watu wawili wenye tabia tofauti na karama tofauti. Hivyo
ukiweka mfumo dume pembeni, ndoa inahitaji uvumilivu wa pande zote
mbili, kusameheana kwa pande zote mbili, kuchukuliana kwa pande zote
mbili, kila upande ukiziachia karama za upande mwingine kuchanua. Hivyo
ikitokea ndoa ikavurugika na kuvunjika, si haki mzigo kubebeshwa upande
mmoja.
Inawezekana Winnie, alifanya makosa na
labda alitembea nje ya ndoa kama wanavyosema wengine, lakini
ukilinganisha na kujitoa kwake kwenye mapambano ya kuleta uhuru wa watu
wa Afrika Kusini, kampeni za kufunguliwa Mandela na kuendeleza jina la
Mandela, wakati Mandela akiwa gerezani, jinsi naye alivyokamatwa na
kufungwa zaidi ya mara 23, uzalendo wake kwa nchi yake, yangefunika
makosa yake madogo na hasa kwa mtu kama Mandela, ambaye anatueleza
aligundua faida ya kutafakari akiwa gerezani.
MTEMBEZI
0 comments: