WAZIRI
wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama
alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa fedha za ahadi ya Rais ya
milioni 50 kila kijiji, ili Watanzania wote wanufaike bila kujali
itikadi zao za kisiasa.
Alisema
hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango(Chadema) aliyetaka kusikia kauli ya
serikali juu ya mgawanyo wa fedha hizo akisema ipo mizengwe kwamba fedha
hizo zitatolewa kwa wanachama wa CCM .
“Serikali itoe kauli fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu gani,” alihoji.
Mhagama
alisema fedha hizo ni ahadi ya Rais aliyotoa wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu ambao Watanzania walichagua Serikali ya CCM.
Alisema serikali inatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Alisema Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi limeanza kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo fedha hizo zitanufaisha Watanzania wote.
Alisisitiza kuwa serikali iko imara kuhakikisha fedha hizo zinanufaisha Watanzania wote.
Awali,
Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM), katika swali la msingi,
alitaka kufahamu ni lini ahadi hiyo ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila
kijiji itatekelezwa.
Alitaka kufahamu pia vijana watapata mgao wao kwa asilimia ngapi.
Mbunge
huyo pia alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuwawezesha vijana
wawe wajasiriamali kwa kuwapa mitaji, mikopo na vigezo gani
vitakavyosimamia na kuwalinda na kuweka usawa wa upatikanaji wa ushiriki
wao katika fursa hizo.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Antony Mavunde alisema ahadi ya Rais ya Sh milioni 50 kwa kila
kijiji itaanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha ujao 2016/2017.
Alisema
utaratibu wa kugawa fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa.
0 comments: