Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko mengine ya kamati za
Bunge kwa kuwaongeza wabunge wapya na kuwahamisha wengine kwenda kwenye
kamati nyingine, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wabunge wakidai
linapunguza ufanisi.
Juzi, Spika Ndugai (pichani) aliwaongeza
wabunge wanne wapya walioapishwa bungeni Aprili 19, kwenye kamati za
Miundombinu; Ardhi, Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Maji; na
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hayo ni mabadiliko ya pili
tangu Bunge la 11 lianze rasmi vikao vyake katikati ya Novemba mwaka
jana, ikiwa ni kipindi kifupi cha mabadiliko ikilinganishwa na Bunge la
Tisa na 10.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na
Mawasiliano cha Bunge, mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni
ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2016, ili
kuhakikisha kila mbunge anakuwa mjumbe wa kamati mojawapo ya Bunge.
“Aidha, mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kadri
itakavyowezekana, Muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge unazingatia aina
za wabunge kwa jinsia, pande za Muungano na Vyama vya Siasa vyenye
uwakilishi bungeni, ujuzi maalumu, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na
matakwa ya wabunge wenyewe,” inasema taarifa hiyo.
Baadhi
ya wabunge jana walipinga mabadiliko ya mara kwa mara ya wajumbe wa
kamati, wakieleza kuwa hayaleti tija na uamuzi huo haufanywi kwa
umakini.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo),
alisema mabadiliko hayo yanaonyesha namna ambavyo Spika Ndugai
“anavyokosa umakini katika uundaji wa kamati hizo”.
“Spika hakuwa makini wakati anaziunda kamati hizo na sina jingine zaidi ya kusema, maana hilo liko wazi,” alisema Zitto.
Mbunge
wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema uundaji wa kamati
kila mara, unatokana na kiongozi huyo kutokuwa na umakini na mara nyingi
anafanya kazi kwa shinikizo la vikao vya chama.
Msabaha alisema
utaratibu wa kuvunja kamati na kuziunda unatokana na vikao vya wabunge
wa CCM, ambavyo humshauri Spika juu ya nini kifanyike ili waweze kuubana
upinzani, ushauri ambao anadai wakati mwingine unakosa tija.
Mbunge
wa Sengerema William Ngeleja (CCM) alisema mabadiliko yanayofanywa
hayana madhara yoyote, kwa kuwa ni jambo la kawaida kufanya maboresho na
kuwataka wabunge kujifunza kupitia mchezo wa mpira ambao kila mtu
anakuwa na namba yake, lakini uwanjani anacheza namba zote.
“Waangalie
mfano wa Profesa Makame Mbarawa ambaye alipewa Wizara ya Maji, lakini
akaondolewa baada ya wiki tatu na kupelekwa kusimamia barabara ambako
ameonyesha uwezo mkubwa, iweje kwa wabunge?” alihoji Ngeleja.
Mbunge
wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema mabadiliko yanayofanywa hayawezi
kuleta tija katika bunge hilo, kwani watu wanashindwa kujipanga vyema
kwa kuwa hawajui kesho itakuwaje.
Lugola alihoji juu ya mafunzo
waliyopata kila kamati, lakini wanabadilishwa bila utaratibu huku
akisema hata kamati ya uongozi inaathirika zaidi, kwani wanapobadilishwa
na kuondolewa wenyeviti lazima kamati ya uongozi ibadilike.
Spika Ndugai hakupatikana jana kueleza kwa kina
mabadiliko hayo. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema siyo msemaji na
Ndugai na ndiye angepaswa kuulizwa jambo hilo.
Katika taarifa
hiyo ya Bunge, Spika Ndugai aliwataka wajumbe wa kamati sita ambazo
hazina viongozi kuwachagua mapema iwezekanavyo kama kanuni za Bunge
zinavyohitaji.
Kamati hizo ni Hesabu za Serikali (PAC)
Mwenyekiti; Kamati ya Nishati na Madini, (Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti); Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii (Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti); Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Mwenyekiti) na
Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Makamu Mwenyekiti.
0 comments: