SERIKALI ya Rais John Magufuli inaelezwa kuendeshwa kwa woga na hofu ya kuumbuliwa hasa kwenye mijadala mikali ya Bunge, anaandika Regina Mkonde na Happiness Lidwino.
Hatua hiyo inaelezwa kuisukuma serikali kufikia uamuzi wa kuzuia kurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge la Jamhuri kupitia Televisheni ya Shirika la Utangazaji nchini (TBC) na pia uamuzi huo kuelekezwa kwenye televisheni binafsi jambo ambalo linaelezwa kuminya uhuru wa habari.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimekuwa vikiitaka serikali kuachana na mpango huo kwa kuwa, vinavyima haki ya wananchi kupata habari jambo ambalo huwasaidia kufanya maamuzi sahihi.
Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Chama cha Wananchi (CUF) – miongoni mwa vyama vya Ukawa- amesema, Serikali ya Rais Magufuli ina hofu kutokana na mijadala ambayo inaweza kuibuliwa na wapinzani na serikali kushindwa kutoa majibu yanayoeleweka.
“Baada ya kuingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano kulikuwa na mabadiliko ikiwemo kuminywa kwa uhuru wa habari, yaani kupata na kueneza habari,” amesema Kambaya na kuongeza;
“Bunge linapooneshwa moja kwa moja, linawejenga wananchi na kuwaonesha jinsi serikali yao inavyowajibika pamoja na kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo inayojadiliwa bungeni.”
Januari mwaka huu Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo aliwasilisha taarifa ya serikali ya kuzuia TBC kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge la Jamhuri kwa madai ya gharama kubwa za urushwaji wa matangazo hayo.
Hatua hiyo iliibua vurugu kubwa ndani ya ukumbi wa bunge na kusababisha kundi la polisi wa kutuliza ghasia kuingia ndani na kuwatoa wabunge wa upinzani ambao walikuwa wanapinga kauli hiyo.
Vurugu hizo zilisababisha kikao kuahirishwa ili kutoa wasaa kwa kamati ya uongozi kukaa na kufanya maamuzi. Hata hivyo, serikali imeendelea na msimamo wake.
Kambaya akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam amesema, kinachofanya na serikali kusitisha kuoneshwa kwa vikao vya bunge moja kwa moja ni hofia ya kushindwa kujibu hoja zinazotolewa na wabunge hususani wapinzani.
“Serikali inajua fika kuwa, haiwezi kujibu hoja za wabunge hasa kwa kipindi hiki kilichotajwa na taarifa za ufisadi, wanazuia kuonesha bunge moja kwa moja ili baadaye wahariri baadhi ya vipande vya matangazo na kuficha hoja za msingi,” anasema.
Amesema, hoja inayosimamia serikali ya kubana bajeti na kusimamia maadili ya bungehaina mashiko kutokana na kwamba, vipo vituo vya runinga binafsi vilivyorusha bunge bila ya serikali kutoa malipo.
Anasema, kitendo cha serikali kutaka kufunga midomo ya viongozi wa upinzani, hakitajenga utawala bora na kuleta masilahi ya taifa.
Kambaya anasema, CUF iko tayari kushirikiana na wananchi, vyombo vya habari binafsi vinavyotaka kuendesha bunge kuishinikiza serikali kuonesha matangazo ya bunge moja kwa moja.
Ni kwa kuwa, kifungu cha 18 cha Katiba ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2005 kinampa haki mtu uhuru wa kujieleza na kutoa mawazo, kutafuta, kupata na kueneza habari bila mipaka.
0 comments: