Monday, 17 March 2014

Kamati ya Zitto yataka ukaguzi IPTL


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeagiza ukaguzi maalumu katika uuzaji wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL na utoaji wa fedha katika akaunti ya Escrow Benki Kuu Tanzania (BoT).
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kamati hiyo kukutana na maofisa wa BoT na kupokea maelezo kuhusu Sh201 bilioni za akaunti ya Escrow na mazingira ya kuchukuliwa kwake.
Fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo na wadau, Tanesco na IPTL baada ya kuibuka mgogoro wa kisheria kutokana na madai kuwa shirika hilo la umeme lilikuwa linalipa gharama kubwa za uwekezaji zaidi ya makubaliano.
Iliamuriwa fedha hizo zihifadhiwe hadi mgogoro utakapokwisha, lakini fedha hizo zikachukuliwa na kampuni iliyonunua IPTL, Pan African Power Solution (PAP).
Mbali na CAG, PAC pia imeagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ianze uchunguzi wa mchakato mzima wa mkataba wa IPTL, umiliki wa kampuni hiyo na uhamishaji wa umiliki kwenda kampuni ya PAP.
"Kamati imeagiza ukaguzi maalumu kutoka PAC ili kupata ukweli. PAC imetoa mpaka mwisho wa mwezi ujao taarifa ya ukaguzi huo iwe imekamilika na kuwataka wahusika wote wa mchakato wa IPTL kusubiri matokeo ya ukaguzi," alisema Zitto na kuongeza: "PAC imetaka pia uamuzi wa mahakama kuheshimiwa."(E.L)
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: