Na Ferdinand Shayo,Arusha. |
Wanafunzi wa Chuo cha Help to Self Help Project wanaosomea masuala ya Uzalishaji wa chakula wakionyesha bidhaa za chakula ikiwemo vitafuno walivyovitengeneza chuoni hapo ikiwa ni njia mojawapo ya mafunzo kwa njia ya vitendo yanayowasaidia kuwa wajasiriamali na kujiajiri wenyewe pindi wanapohitimu mafunzo.Picha na Ferdinand Shayo |
Mkuu wa Chuo Ufundi na Mafunzo cha Help to Self Help Bi.Delneva Makundi Akifafanua jambo kwa mwandishi |
Katika
ulimwengu wa sasa wenye changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na ushindani wa
kila namna ujasiriamali unabaki kuwa dhana pekee inayoweza kuwakomboa vijana
kiuchumi na kuwawezesha kutimiza malengo na ndoto walizonazo.
Kutokana na
kukithiri kwa idadi kubwa ya vijana wanaohitimu katika ngazi mbali mbali za
elimu hasa elimu ya msingi,sekondari na Chuo
ile hali hawana ajira na kuishia kukaa
mitaani kutokana na elimu waliyoipata iliwaandaa kuajiriwa maofisini na sio
kujiajiri,ni ukweli usiopingika kwamba elimu ya ujasiriamali inahitajika kwa
kiasi kikubwa ili kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi.
Juhudi kubwa
inatakiwa ifanyike kuanzia mashuleni kutoa elimu hiyo ili kuwafanya vijana
wafikirie juu ya kuwa wazalishaji zaidi kuliko kutegemea nafasi finyu za kuajiriwa maofisini hali inayopelekea
idadi kubwa ya wasio na ajira.
Mafanikio ni shilingi yenye pande
mbili kuajiriwa na kujiajiri ,vijana wasifikiri kuwa kuajiriwa ndio njia pekee
ya kufanikiwa pia wajue kuwa kuna mafanikio ya kiuchumi nje ya ajira
na haya ni kwa wale walioamua kujiajiri kwa kuanzisha miradi mbali mbali ama
biashara na huo ndio ujasiriamali wenyewe.
Mese Muro ni
Makamu Mkuu wa Chuo cha Help to Self Help
Project kilichopo jijini Arusha kinachojishughulisha na kutoa elimu ya
ujasiriamali pamoja na mafunzo ya ufundi anaeleza kuwa wamekuwa wakitoa elimu
juu ya kutengeneza bidhaa mbali mbali hasa za chakula na usindikaji ujuzi ambao
umewasaidia vijana wengi kujiajiri
kupitia maarifa waliyoyapata chuoni hapo.
Bi.Mese
anafafanua kuwa mafunzo ya ujasiriamali wanayoyatoa yamekuwa yakilingana na
uhitaji ulioko katika soko la ajira hivyo kuwawezesha wahitimu kupata ajira
katika taasisi mbali mbali na wengine kujiajiri kutokana na uwezo wanaojengewa
chuoni hapo ambao huwasaidia kuyamudu maisha na kujitegemea kiuchumi.
“Tunawafundisha
vijana namna ya kutengeneza bidhaa ,kuzifungasha na tunawaelekeza namna ya
kuyafikia masoko pamoja na namna bora ya kuwahudumia wateja yaani customer
care” Alisema Makamu Mkuu huyo wa chuo
Bi.Mese
anawataka vijana kutokuwa wamachinga wa bidhaa za nchi za nje bali
ajifunze kuteneneza bidhaa na kuziuza
kwani huo ndio ubunifu unaohitajika kwa
vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Akitolea
mfano fani ya Uzalishaji wa chakula ambayo
ni fani mama yenye kuhitajika na kila mtu duniani ili aweze kuishi ni lazima apate chakula
ambapo wamekua wakitoa mafunzo juu ya upishi,usindikaji wa vyakula na uandaaji
wa vinywaji ambapo imewasaidia vijana wengi kuajiriwa kwenye mahoteli na
wengine kufungua biashara zao na kunufaika kiuchumi.
Mbali na
hayo wanatoa mafunzo ya umeme,ushonaji
na mengine ambayo anaamini yanamsaidia kijana kujikomboa kiuchumi.
Vijana
wanakuja na shabaha kuwa baada ya kuhitimu wataweza kupata hela kupitia taaluma
zao na sisi tunahakikisha hilo linafanikiwa kwa kuwapa mafunzo bora
yaliyojikita kwenye vitendo zaidi kuliko
nadharia ili waweze kuhimili ushindani ulioko kwenye soko.
Pia
anashauri serikali kufanya kitu kwa ajili ya vijana ikiwemo kutengeneza fursa
kwani vijana wengi wanajitambua na wanapenda maendeleo.
Vedastus
David Sibula ni Mratibu wa Chuo cha Help to Self Help Project anasema kuwa vyuo
vya ufundi vinasaidia kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo pia vitapanua
wigo wa ajira mfano kutengeneza mikate,soseji na juisi badala ya kuagiza kutoka
nchi za nje.
Mratibu huyo
anaeleza kuwa elimu ya ufundi imekua ikiwasaidia
vijana kwa kiasi kikubwa kukabiliana na maisha na kuyamudu kwa kufanya kazi na
kujiingizia kipato ndani na nje ya ajira ukilinganisha na elimu nyingine.
“Ni nadra
sana kukuta kijana amemaliza VETA amekaa mtaani hana cha kufanya lakini utakuta mtu amaliza chuo kikuu degree na kazi hana” Vedastus
“Kuna dada aliyesoma hiki chuo sasa hivi anatengeneza
keki kwenye masherehe kajiajiri amefanikiwa kaajiri wafanyakazi,ana nyumba
nzuri na gari kwa ujumla anayamudu maisha ,huo ni mfano mzuri na wako wengi
waliotoka hapa na kujiajiri” Alisema Mratibu huyo
Eugene John
ni Mhasibu wa chuo hicho anaeleza kuwa tatizo lililoko kwenye soko la ajira sio
ajira bali ni kukosekana kwa ubunifu kunakowapelekea watu wengi kufanya
biashara ya aina moja kwa kuigana na mwisho kujikuta wakikosa wateja.
Hivyo
amewataka Wajasiriamali kuwa wabunifu na kufanya vitu vya kitofauti ili
kuliteka soko la biashara lililojaa ushindani mkubwa kwani kwa kufanya hivyo
watafanikiwa kiuchumi.
Kwa upande
wao wanafunzi wanosoma katika Chuo hicho katika kozi ya uzalishaji wa chakula Saidi Swedy na Salma Fadhili wanaeleza kuwa
wamekuwa wakifundisha namna ya kutengeneza bidhaa kama keki,soseji,yogati kuzifungasha na kuzipeleka masokoni ambapo na
kuziuza jambo ambalo limekua
likiwasaidia kujiingizia kipato ile hali bado wanasoma.
Licha ya
kuuza bidhaa zao nje ya chuo pia wamekua
na utamaduni wa kuwauzia wanafunzi wenzao.
“Tangu
nimeanza chuo nimepata mafanikio hata kabla ya kufikia muda wa kuhitimu nimekua
nikipika vitafuno na kuviuza,siku za jumamosi huwa nafanya kazi kwenye mahoteli
na vikundi vinavyopika kwenye masherehe hivyo kujipatia fedha ambazo huzitumia
kujikimu ukizingatia kuwa mimi najitegemea inanisaidia kulipa kodi,ada na
mahitaji yangu muhimu” Alisema Saidi
Salma
Fadhili anaongeza kuwa siku za likizo ya chuo huzitumia kupika vitafuno na kuviuza mashuleni na taasisi
mbali mbali na kupata faida ambayo
imemsaidia kupunguza utegemezi kwani hujipatia mahitaji yake muhimu bila
kulazimika kuwafuata wazazi ama kutumia njia za mkato.
Anawashauri
vijana wanaomaliza shule ngazi ya msingi na sekondari kutokukata tama bali kujiingiza
katika matendo mabaya ya wizi,umalaya,matumizi ya madawa ya kulevya na badala
yake wajiunge na vyuo vya ufundi vitakavyowasaidia kupata mafunzo yatakayowawezesha kuyamudu maisha.
0 comments: