Tuesday, 13 May 2014

USIOMBE GONJWA HILI LIKUPATE, TUJUMUIKE PAMOJA KUMSAIDIA MAMA HUYU


MARY Izengo (52), mkazi wa Kijiji cha Umanda- Msalala, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza anateseka kiasi cha kutamani afe kufuatia gonjwa la ajabu alilonalo huku akisema ndugu, wakiwemo watoto wake wamemtenga.
Mary Izengo anayesumbuliwa na gonjwa la ajabu.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya Wadi Namba 23, Jengo la Sewa Haji kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, mwanamke huyo alisema usiombe gonjwa hilo likupate kwani ugonjwa unaomkabili ni wa uvimbe mkubwa usoni ambapo unamtesa kwa kipindi kirefu huku akionekana  kero kubwa katika jamii.
ATOA HISTORIA YAKE HUKU AKILIA
Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye wakati akizungumza na Uwazi mara kwa mara alikuwa akilia, alisema:
“Nilizaliwa mwaka 1962 katika Kijiji cha Umanda Msalala, wilayani Sengerema nikiwa mzima wa afya wala sikutegemea kama siku moja ningekuja kuwa katika hali hii.
“Nikiwa na umri wa miaka mitano ndipo nilipoanzwa na tatizo hili. Ulianza kwa kutoka vipele vidogovidogo mdomoni ambavyo viliniletea maumivu makali. Wazazi walinipeleka hospitali nikatibiwa kwa kuchomwa sindano lakini bila mafanikio.
“Hali ilipozidi kuwa mbaya, wazazi hawakukata tamaa, wakanipeleka Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, lakini nako pia  ikashindikana, nikarudishwa nyumbani.
“Hali yangu iliendelea kuwa mbaya zaidi nikachangiwa fedha na kupelekwa Hospitali ya Bugando, Mwanza ikashindikana pia, nikarudishwa tena nyumbani.
Mary Izengo akiwa amelazwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Kwa bahati nzuri, alijitokeza mwanaume na kunioa akisema hatajali ugonjwa wangu na baadaye wazazi wangu walifariki dunia,” alisema mwanamke huyo akiendelea kulia.
Akaendelea: “Nilizaa watoto wawili kwa mume wangu na alinipenda sana na kunisaidia kwa kadiri ilivyoweza kutokana na kipato chake. Alikuwa mkulima wa jembe la mkono.
“Ila baadhi ya ndugu zake walipoona sura yangu inazidi kubadilika walimshauri anifukuze eti ili ugonjwa wangu usije ukaenea katika ukoo lakini aliwakatalia na kuzidisha mapenzi kwangu jambo ambalo lilinitia moyo.
“Mwaka 2011 mume wangu alifariki dunia na kuniachia watoto. Nililia sana kwani nilijua nitateseka kupita kawaida. Baada ya baba yako kufa, watoto nao wakanikimbia wakisema ugonjwa wangu ni uchuro.
“Nikawa naishi peke yangu. Mara nyingi nilikuwa nikishinda njaa kama majirani hawakuniletea chakula, nilitamani kujiua  na nikasema bora nife tu.
AENDA MKUTANO WA MBUNGE, APATA MSAADA
Mary aliendelea kusema kuwa, siku moja alijikuta akisukumwa kwenda kwenye mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Nyang’wale wilayani Geita, Mhe. Ahmed Nassor Amar ‘Gulamali’.
“Haikuwa kawaida yangu kushiriki mikutano, lakini siku hiyo nilikwenda. Mwisho wa mkutano, mbunge aliniona akanihurumia sana na kuniambia nije Muhimbili nipatiwe matibabu, akanipa shilingi laki tatu.
“Ndipo Aprili mwaka huu nikamtafuta msamaria mwema, akanileta hapa Muhimbili ambapo madaktari wamenipokea vizuri sana,” alisema mama huyo.
“Madaktari walinifanyia uchunguzi na wakanieleza kwamba kuna mshipa unapitisha damu kwa wingi ndiyo maana nimevimba hivi, wakasema matibabu yake hapa nchini haiwezekani mpaka India. Kwa hiyo kwa sasa nasubiri kama nitaweza kwenda huko.
ASHANGAZWA NA NDUGU
“Kinachonishangaza na kunisikitisha ni kwamba, hapa Dar es Salaam nina kaka yangu, nilipofika tu hapa hospitali nilimuomba muuguzi simu nikampigia kumjulisha kuwa naumwa nipo Muhimbili. Miaka mingi hatujaonana akafikiri kuwa ugonjwa wangu ni wa kawaida.
“Alipokuja na kuniona alitokwa machozi na kuondoka. Kuanzia hapo kila nikimpigia simu hapokei,” alisema mama huyo.
Mary anaomba msaada ili aweze kupata fedha zitakazomuwezesha kwenda India kutibiwa. Ukitaka kumsaidia tuma fedha kwa namba 0683 406 680 ya afisa ustawi wa jamii aliye karibu naye
-GPL
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: