- KWA kawaida marais wakishaingia madarakani wanakuwa na Katibu Mkuu Kiongozi waliyemkuta kwa kipindi cha mpito, lakini baadaye wanakuwa na Katibu Mkuu Kiongozi wakwao, kwa hiyo siyo jambo la ajabu kwangu....
Balozi Sefue aliyasema hayo wakati akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi baada ya kumalizika kwa hafla ya kuwatunuku vyeti vya shukrani wadau mbalimbali wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, akiwamo Balozi Sefue, vilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Nipashe ilitaka kujua kwa undani kilichochangia kuondolewa kwake katika wadhifa huo aliodumu nao kwa siku 65 baada ya Dk. Magufuli kuingia Ikulu.
“Kama unajua ilivyo kwenye historia, kwa kawaida marais wakishaingia madarakani, wanakuwa na Katibu Mkuu Viongozi waliowakuta kwa kipindi cha mpito, lakini baadaye wanakuwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa kwao, kwa hiyo siyo jambo la ajabu kwangu,” alisema.
Alipoulizwa juu ya maisha ya uraiani, alisema: “Hayo wakati wa kuyazungumza bado…kuhusu majukumu mengine nikipangiwa mtayasikia.
” Balozi Sefue aliteuliwa kuendelea na nafasi hiyo Desemba 30, mwaka huu, baada ya kuitumikia wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Dk. Jakaya Kikwete.
Kuhusu utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli, alisema: "Inafanya kazi nzuri sana na kwamba Watanzania wanapaswa kujiona wenye bahati. Mtu yeyote ambaye anaitakia nchi hii mema, hawezi kuacha kukiri kwamba chini ya uongozi wa Dk. Magufuli, tumeona mabadiliko makubwa yanayoashiria neema kwa Tanzania yetu.
” Balozi Sefue ambaye atakumbukwa na waandishi wa habari nchini kwa kutoa ushirikiano na kujibu maswali yao muda wowote bila ubaguzi, alisema Tanzania itapiga kasi kubwa ya maendeleo akijenga juu ya yale yaliyofanywa na walio nyuma yake, lakini kasi yakuibadili Tanzania ni kubwa.
"Bila shaka Mwenyezi Mungu atatusaidia tutafanikiwa, Watanzania wote tumuombee Rais wetu aendelee kutuongoza tufikie nchi nzuri kiuchumi,” alisema.
Baada ya Balozi Sefue kuondolewa katika wadhifa huo, Rais Dk. Magufuli alimteua Balozi Mhandisi John Kijazi, kushika nafasi hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Kijazi alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India.
Chanzo: Nipashe
0 comments: