Inaandikwa na Dkt. Ramadhani K. Dau
*Ilikuwa
siku ya Jumamosi tarehe 23 Disemba 2017, majira ya saa 5 usiku kwa saa
za Malaysia nilipopata ujumbe mfupi wa sms kutoka kwa *Sheikh Issa
Othman*, maarufu Mufti wa London, Imam wa Masjid Maamur ukiniarifu msiba
wa mzee wetu Sheikh Ahmed Islam. Ujumbe wake ulikuwa mfupi sana: “Mzee
wetu Ahmed Islam amefariki sasa hivi. Maiti inaletwa msikitini hivi
sasa. Maziko kesho In Shaa Allah. Innallillahi Wainnaillahi Raajiuun”.
Mara
tu baada ya kupata taarifa hiyo na baada ya kumtakia maghfira mzee
wetu, nikajua kuwa kwa mara nyingine tena umeniangukia wajibu wa
kuandika Taazia ya mtu ambaye namfahamu, namheshimu na alikuwa na
ukaribu sana na mimi. Nimeshawahi kuandika huko nyuma kuwa kuandika
Taazia ni jambo zito na gumu sana.
Kila
niandikapo hutamani sana Taazia hiyo iwe ndio ya mwisho. Lakini kwa
mipango Yake Mwenyezi Mungu, najikuta nashindwa kukwepa wajibu huo. Hata
hivyo, mara hii nilidhani ningeweza kuukwepa wajibu huo kwa kumuomba
rafiki yangu na ndugu yangu mwanahistoria maarufu *Sheikh Mohamed Said*
aandike Taazia hiyo nami nilikuwa tayari kumpa maelezo yoyote ambayo
yangemsaidia katika uandishi wake.
Pamoja
ya kuwa alikubali kuifanya kazi hiyo, Mohamed alisisitiza kuwa lazima
na mimi niandike. Kwa jinsi ya msisitizo aliouweka Sheikh Mohamed,
nimejikuta kwa mara nyingine tena nalazimika kuandika Taazia hii huku
nikiwa na moyo wa huzuni sana kwa kuondokewa na mzee wangu ambaye
alikuwa mithili ya baba yangu mzazi.
Marehemu
mzee Ahmed Islam ana mambo mengi na sura nyingi. Wapo wanaomfahamu kama
ni miongoni mwa wazee maarufu na viongozi katika jamii ya Waislamu,
wapo wanaomfahamu kama mtaalamu wa masuala ya Rasilimali Watu (Human
Resources) na wapo wanaomfahamu mzee Ahmed Islam kama mwana michezo
mahiri.
*Marehemu
mzee Ahmed Ijhad Islam* alizaliwa Zanzibar tarehe 22 Disemba 1930 akiwa
ni mtoto pekee wa Sheikh Ijhad Islam na bibi yetu Bi Maryam Mussa. Kwa
bahati mbaya, mzee Ijhad Islam alifariki wakati mzee Ahmed akiwa mdogo
na hivyo akalelewa na mama yake. Baada ya msiba huo, bibi yetu Bi Maryam
aliolewa na kupata mtoto mmoja wa kike ambaye jina lake ni Zerah.
Baada
ya kumaliza masomo yake ya msingi na Sekondari kwenye Government School
(sasa Ben Bella) Zanzibar, mwaka 1957 marehemu mzee Ahmed Islam
alikwenda Cornwall, Uingereza kuchukua masomo katika fani ya Mawasiliano
yaani Telecommunications. Wakati huo alikuwa ameajiriwa na kampuni ya
Cable and Wireless (C&W) ambako alikuwa Meneja Msaidizi (Assistant
Manager). Baada ya kurudi masomoni, marehemu aliendelea na kazi yake na
baada ya kampuni ya C&W kumezwa na Shirika la Posta na Simu la
Afrika Mashariki (East African Post and Telecommunication), mzee Islam
akahamishiwa Dar es Salaam mwaka 1970.
Akiwa
Dar es Salaam mzee Islam alifanyakazi katika Shirika hilo na baada ya
mgawanyiko yakaundwa Mashirika mawili tofauti; Shirika la Posta (TPC) na
Shirika la Simu (TTCL). Marehemu mzee Islam alihamishiwa TTCL hadi
alipostaafu mwaka 1980 akiwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Rasilimali
Watu yaani *Director of Manpower*. Baada ya kustaafu, marehemu
alifanyakazi Ubalozi wa Ufaransa kwa mkataba wa miaka 3. Wakati wa uhai
wake, mzee Islam amefanya mengi katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja
na uongozi wa dini, ujenzi wa nchi, uendelezaji wa michezo na utoaji
nasaha kwa Taasisi na vijana mbalimbali katika masuala ya ndoa na
kujiendeleza kwenye elimu ya juu.
*Kwa
upande wa dini, marehemu ametoa mchango mkubwa sana*. Miongoni mwa
matunda ya kazi yake ni usimamizi wa ujenzi wa Masjid Maamur iliyopo
Upanga, Dar es Salaam. Kwa wanaokumbuka vizuri jiografia ya Upanga, pale
palipojengwa Masjid Maamur hapakuwa na msikiti. Lakini kwa kushirikiana
na wazee wenziwe marehemu mzee Islam aliweza kusimama kidete katika
kusimamia ujenzi wa Masjid. Kana kwamba hiyo haitoshi, mwaka 2013,
marehemu mzee Islam alichangia kwa kiasi kikubwa usimamizi wa ukarabati
mkubwa wa msikiti huo kwa ufadhili mkubwa wa kampuni ya Oil Com.
Mbali
na Masjid Maamur, marehemu mzee Islam pia alitoa mchango mkubwa sana
katika ujenzi wa Masjid Ngazija hapa Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya
sana tokea ukoloni hadi leo, katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Central
Business District), hakuna msikiti wowote mkubwa wala mdogo zaidi ya
msikiti wa Ngazija. Lakini msikiti huo ambao ulijengwa wakati wa ukoloni
ulikuwa ni mdogo sana kiasi cha kutokidhi mahitaji ya Waumini. Hivyo
basi kwa kushirikiana na viongozi wengine kama vile marehemu *Sheikh
Aboud Maalim, marehemu Profesa Haroub Othman Miraji, Sheikh Saidi
Kassim, Habibu Nuru, AbdulHamid Mhoma* na wengineo, marehemu mzee Islam
alishiriki kusimamia ujenzi wa msikiti mpya wa Ngazija ambao kwa sasa
una ghorofa 3 na ndio msikiti pekee uliopo Dar es Salaam Central
Business District. Pamoja na usimamizi wa ujenzi wa misikiti, mzee Islam
ametunga vitabu mbali mbali vya dua na nyiradi na alikuwa mmoja wa
wasimamizi wa uradi Masjid Ngazija kila Alhamisi.
Mchango
wa marehemu mzee Islam katika kuwaendeleza vijana wa Kiislamu kielimu
ni mkubwa bila kifani. Nina hakika si watu wengi wanaofahamu kuwa *mzee
Ahmed Islam ndiye ambaye aliyefanikisha kupatikana kwa kiwanja ambacho
kwa sasa imejengwa shule ya Sekondari ya AlHaramain jijini Dar es
Salaam*. Naishauri BAKWATA ambayo ndio Wamiliki wa Shule ya AlHaramain
wathamini mchango wa mzee Ahmed Islam kwa kulipa jina lake moja ya
madarasa au kumbi za shule. Aidha mzee Islam alikuwa mstari wa mbele
kwenye Taasisi ya Muslim Solidarity Trust Fund katika kusimamia nafasi
za masomo za vijana wa Kiislamu wanaokwenda kusoma Uturuki kwa ufadhili
wa Benki ya Maendeleo ya Kiislam (Islamic Development Bank) iliyopo
Jeddah, Saudi Arabia. Chini ya ufadhili huo, kwa karibu miaka 30 sasa
Benki hiyo imekuwa ikifadhili vijana wa Kiislamu 15 kwenda kusoma masomo
ya Uhandisi (Engineering) na Utabibu (Medicine) kwenye Vyuo Vikuu
nchini Uturuki. Miongoni mwa watu walionufaika na mpango huu ni *Dr.
Hussein Mwinyi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr.
AsanteRabi Kighoma Malima wa Chuo Kikuu cha Northeastern Marekani, Dr.
Mashavu, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, Dr. Munawwara Kaguta
daktari wa hospitali ya Aga Khan* na wengine wengi.
Moja
ya mafanikio makubwa ya jitahada za marehemu mzee Islam ni uvumbuzi
ambao ulifanywa mwezi Agosti 2014 na Dr. AsanteRabi Kighoma Malima
ambaye alivumbua kifaa cha kuweza kubaini maradhi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na saratani (cancer) yakiwa katika hatua za awali kabisa.
Kutokana na uvumbuzi wa kifaa hicho ambacho amekiita Biolom, Dr. Malima
alipewa tuzo na Gavana wa jimbo la Massachusetts, Bwana Deval Patrick.
Haya ni matunda ya mzee wetu Ahmed Islam ambayo yameiletea sifa kubwa
sana nchi yetu katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Aidha
mwaka 2002, mzee Islam *aliishawishi Taasisi ya Muslim Aid ya London
kuja kujenga maabara 3 za kisasa katika shule ya Sekondari ya Twayyibat
iliyopo Temeke Dar es Salaam*. Katika kipindi hicho hicho, kwa kupitia
Muslim Aid, mzee Islam pia alifanikisha ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi
katika shule ya Sekondari ya Sotele, Kisiju Mkoa wa Pwani. Harakati za
marehemu mzee Islam kuwasaidia vijana katika kutafuta elimu hazikuanzia
Dar es Salaam.
*Wakati
akiwa Zanzibar, marehemu alikuwa akiwahimiza sana vijana kusoma na yeye
binafsi alikuwa akijitolea kuwapa vijana mafunzo ya ziada (tuition)
usiku kwa kutumia taa za kibatari*.
Marehemu
mzee Islam alikuwa Mcha Mungu sana. Pamoja na kuwa na umri mkubwa wa
miaka 87 na kuandamwa na maradhi ya miguu, kamwe hakuacha kuswali swala
zote katika msikiti Maamur. Siku zote alikuwa wa kwanza kuingia
msikitini na kuswali kwenye kiti msitari wa mbele. Mwaka 1997,
*nilibahatika kusafiri kwenda Umra na marehemu mzee Islam* wakati
Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lilipofanya safari yake ya kwanza
kwenda Jeddah, Saudi Arabia. Katika safari yetu walikuwepo *marehemu
mzee Ahmed Rashad Ali, marehemu Siraju Juma Kaboyonga na mkewe marehemu
Jaji Madina Muro, marehemu Prof. Haroub Othman, marehemu Balozi Selemani
Hemedi, Dr. Idris Rashid, Jenerali Ulimwengu, mama Fatma Maghimbi, Mhe
Hamad Rashid, mwanahistoria Sheikh Mohamed Saidi* na wengineo. Wengi
walimshuhudia takriban kwa siku zote tulizokuwa safarini, marehemu mzee
Islam alikuwa anaamka usiku kufanya ibada.
Mzee
Islam alikuwa mtu wa watu na alikuwa mwepesi sana wa kusaidia watu
wenye matatizo. Milango ya nyumba yake ilikuwa wazi saa zote ambapo watu
wa rika zote walikuwa wanaenda kila siku kutaka misaada au ushauri.
*Mzee Islam alikuwa jeshi la mtu mmoja na alikuwa zaidi ya Taasisi*.
Hapa ntasimulia matukio mawili kati ya matukio mengi sana ambayo
yanaonesha ukarimu na utayari wa marehmu katika kusaidia watu.
Siku
moja mama mmoja kutoka mkoa wa Kilimanjaro alikwenda nyumbani kwa mzee
Islam akiwa na watoto wa kike watatu ambao wote walikuwa yatima. Baada
ya kueleza matatizo yake na ugumu wa maisha ya kulea wale mayatima,
marehemu mzee Islam akamshauri wale watoto wabaki kwake na yeye
atachukua jukumu la kuwalea na kuwasomesha. Yule mama akakubali rai ile.
*Hivi niandikavyo Taazia hii*, mtoto mmoja amemaliza masomo ya Shahada
ya kwanza katika Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa
sasa anafanyakazi Tanga. Mwingine amemaliza Shahada ya Uzamili katika
fani ya Uthamini vifaa vya ujenzi (Masters Degree in Quantity Survey)
kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam. Na wa mwisho hivi sasa
anachukua Stashahada (Diploma) ya Uhasibu.
Tukio
lingine lilitokea mwaka 1991 wakati kijana mmoja alipokwenda nyumbani
kwa mzee Ahmed Islam kumuomba msaada wa kwenda masomoni Ujerumani. Kama
ilivyo kawaida yake, mzee Islam hakusita na alisimamia uchangishaji wa
fedha kwa ajili ya safari masomo ya kijana huyo. *Leo hii, kijana huyo
ni daktari bingwa nchini Ujerumani*. Mifano kama hii ipo mingi na nafasi
haitoshi kuisimulia yote.
Kwa
upande wa michezo, mzee Islam hakuwa nyuma. Wakati wa uhai wake,
alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu kiasi cha kuitwa mchawi wa
mchezo huo. Alipokuwa Zanzibar alicheza timu ya Vikokotoni na timu ya
Taifa ya Zanzibar. Akiwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar, mzee
Islam alishiriki katika mashindano kadhaa ikiwemo mashindano maarufu ya
kombe la Gossage akicheza namba 10. Mwaka 1952 timu ya Taifa ya Zanzibar
ilifika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika Nairobi Kenya na
kushika nafasi ya pili baada ya kuzifunga timu za Tanganyika na Uganda.
Pamoja wachezaji wengine, timu ya Zanzibar iliwakilishwa na marehemu
*mzee Ahmed Islam, marehemu mzee Abdul Majham Omar, Mzee Mwinyi
(Mpiringo), Seif Rashid na Maulid Mohamed (Machaprala)*. Pamoja na
umahiri wake wa kucheza mpira wa miguu, mzee Islam alikuwa mchezaji
hodari wa Kriket na mpira wa magongo (hockey). Kama ilivyo kwenye mpira
wa miguu, marehemu mzee Islam alichezea timu za Taifa za Zanzibar kwenye
Cricket na Hockey.
Wakati
wa uhai wake, mzee Islam alikuwa mzungumzaji wangu sana sio tu kwenye
masuala ya jamii lakini pia masuala ya michezo. *Mimi na marehemu
tulikuwa tunakubaliana kwenye mambo mengi sana isipokuwa mambo mawili
ambayo tulikubaliana kutokubaliana*. Kwanza kwenye upenzi wa mpira kwa
timu za hapa nyumbani *marehemu mzee Islam alikuwa mpenzi mkubwa wa
Yanga wakati mimi ni mpenzi wa Taifa Stars. Kwa upande wa timu za nje ya
nchi, mzee Islam alikuwa anaipenda sana Manchester United. Bahati mbaya
sikuwahi kumuuliza sababu ya yeye kuipenda Manchester United. Kama
sababu ni kutembelea jiji la Manchester wakati alipokuwa masomoni
Uingereza, basi nilitarajia angeipenda Manchester City kwa sababu klabu
hiyo ndio ipo katika jiji la Manchester wakati timu ya *Manchester
United ipo shamba kabisa kwenye kitongoji kidogo kinachoitwa Old
Trafford. Kwa hapa nyumani, kitongoji cha Old Trafford mfano wake ni
kama vile Dar es Salaam na Ruvu Darajani pale panapouzwa samaki wakavu
au mbele kidogo kwenye kijiji cha Vigwaza*. Wenyewe Waingereza wanasema
there is only one team in Manchester (Manchester kuna timu moja tu)
ambayo ni Manchester City. Pia wanao msemo wao unaosema there is only
one football team in London; the Gunners! (London kuna timu moja tu ya
mpira wa miguu; washika Bunduki). Najua Balozi Saleh Tambwe na Balozi
Juma Mwapachu watalipinga hili. Lakini haya si maneno yangu.
Niliwahi
kuandika mapema mwaka huu kuwa kutokana na vifo vilivyoongozana vya
wazee wa Dar es Salaam, jiji letu limebaki kuwa na ukiwa. *Mwaka huu
tumeshuhudia kuondokewa kwa Kamanda Dr. Mohamed Chiko, mzee Iddi
Sungura, mzee Issa Ausi (smart boy), Ali Bob, mzee Kitwana Selemani
Kondo, Kleist AbdulWahid Sykes na sasa mzee Ahmed Islam*. Jiji la Dar es
Salaam limegubikwa na huzuni kubwa. Lakini kwa sababu kifo ni faradhi
hatuna budi tuikubali hali hiyo.
Mzee
Islam ametangulia lakini ameacha simulizi ambazo zitazungumzwa kwa
miaka mingi sana baada ya yeye kuondoka. Wakati wa uhai wake, marehemu
mzee Islam na mama yetu Bi Rukia Ahmed Iddi ambaye alifariki 1989
walijaaliwa kupata watoto sita ambao ni *Islam, Biubwa, Mohamed (maarufu
Eddy), AbdulRahman, Abubakar na Mussa*. Tunamwomba Mwenyezi Mungu
Amrithishe mzee wetu Ahmed Islam Jannat Firdous kama Alivyosema Mwenyewe
kwenye Quran Sura 23 Aya 1-11 pale Alipozitaja sifa za watu wema kisha
Akamalizia kwa kusema Atawarithisha Firdous na wataishi humo milele.
Pia tunamwomba Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema na Atukutanishe na mzee wetu Ahmed Islam kwenye Firdous.
Aaamiin.
0 comments: