Monday, 28 April 2014

SOMA HISTORIA YA SHUJAA HUYU WA BONGO FLEVA ALIYESAHAULIKA

JAMES Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ siyo jina geni katika gemu la Bongo Fleva lakini ni wangapi wanamkumbuka na wanautambua mchango wake katika gemu la Bongo Fleva? Ungana nami ili kumjua kwa kina.
James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ (kushoto katika picha) enzi za uhai wake.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
James Dandu au kwa jina lingine Cool James Massive ‘CJ Massive’ alizaliwa Julai 5, 1970, Mwanza nchini Tanzania. Alisoma shule ya Msingi Kurasini na baada ya hapo, yeye, mama yake na ndugu zake walihamia jijini Stockholm, Sweden alikoishi kwa kipindi kirefu.
ALIVYOINGIA KWENYE GEMU
James Dandu aliingia rasmi kwenye sanaa ya muziki mwaka 1988 akiwa jijini Stockholm ambapo alitoa singo kadhaa zikiwa katika staili ya Euro-House. Mwaka 1992 aliachia albamu yake ya kwanza ambayo hata hivyo haikupata mafanikio makubwa.
Mwaka 1993, aliungana na msanii mwingine kutoka Afrika Mashariki, Andrew Muturi na kuunda kundi lililokwenda kwa jina la Swahili Nation. Wasanii wengine wawili wakajiunga kwenye kundi hilo.
Baadaye, James Dandu alijitoa kwenye kundi hilo na kuungana na Mkongomani, Jose Masena ‘Black Teacher’ na kutoa albamu mbili zilizowatambulisha vyema sehemu mbalimbali; Undercover Lover (1992) na Zooming You (1995) iliyokuwa na wimbo ulioitwa Dr. Feel Good. Wakapata mafanikio makubwa na kuingiza mkwanja wa maana.
AREJEA BONGO KWA KISHINDO
Kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na mwenzake, Black Teacher, Mtoto wa Dandu aliamua kurudisha majeshi nyumbani kwa lengo la kuja kuibua na kuinua vipaji Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.
Aliporudi Bongo, alikuja na staili mpya ya uimbaji wa nyimbo za taratibu (R&B) ambao haukuwa umezoeleka sana kwa kipindi hicho. Akajipatia umaarufu mkubwa ndani ya kipindi kifupi.
Hakuishia hapo, aliendelea kuingiza ubunifu katika kazi zake, akawa anachanganya R&B ya kisasa, Rhumba na Ndombolo (staili iliyokuwa maarufu sana nchini Zaire kipindi hicho). Akatoa albamu nyingine kama Soft Like a Pillow (1997), Bi Harusi (1998) na Sukuma Land (2002).
Miongoni mwa ngoma ambazo mpaka leo zikipigwa lazima watu watulie ni Sina Makosa ambayo aliurudia wimbo wenye jina hilohilo uliopigwa na Les Wanyika kutoka Kenya. Ngoma hii ilimtambulisha kinoma Afrika Mashariki yote, hususan nchini Kenya.
Pia alifanya remix ya wimbo wa Mamu akiwa na mkali Madilu System ambao ama kwa hakika ulibamba mbaya!
TUZO ZA KILI
Mwaka 1999, James Dandu aliamua kuanzisha tuzo alizoziita Tanzania Music Awards ambazo hivi sasa zinajulikana kama Kili Music Awards baada ya kuanza kudhaminiwa na bia ya Kilimanjaro.
James Dandu ndiye aliyefanikisha usajili wa tuzo hizo kwa kushirikiana na Basata chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni (kipindi hicho).
KIFO CHAKE
Mtoto wa Dandu alifariki Agosti 27, 2002, kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam, nyota yake ikiwa inang’ara kinoma na kuzusha simanzi kubwa miongoni mwa mashabiki wake, hususan wanawake ambao walikuwa mashabiki wake wakubwa.
Akaenda kuzikwa nyumbani kwao, Mwanza. Wakati anakufa, alikuwa bado hajamaliza kurekodi kazi zake mpya katika Studio ya Master Jay. Aliacha watoto wawili wakiwa bado wadogo pamoja na mjane, Devotha.
MIAKA 12 BAADA YA KIFO CHAKE
Ni miaka 12 sasa imepita tangu Mtoto wa Dandu aliporejea kwenye makazi yake ya milele. Swali ambalo mimi na wewe tunapaswa kujiuliza, je, anapewa heshima anayostahili hata kama alishatangulia mbele za haki? Familia yake wakiwemo wanaye Caroline-Jamie ’Malaika’ aliyezaliwa mwaka 1994 na Michael James Junior aliyezaliwa 1997 wananufaika na matunda ya kazi za baba yao? Nawashauri waandaaji wa Tuzo za Kili wamuenzi James Dandu japo kwa tuzo ya heshima!
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: