Monday, 5 May 2014

Nguruwe kupigwa risasi


Wanaharakati wamepinga vikali kuwaua Nguruwe wakisena ni kinyume na haki za wanyama
Maafisa wa mji wa Shivpur nchini India wamejikuta matatani kwa kuwataka watu wanaomiliki bunduki kuwapiga risasi Nguruwe wanaotembea ovyo mjini humo.
Wakazi waliamrishwa kubeba bunduki zao pamoja na leseni zao kuthibitisha wana idhini ya kumiliki bunduki ili kuweza kushiriki zoezi hilo. Taarifa hii ni kwa mujibu wa jarida la Hindustan Times.
Maafisa wa utawala walisema kuwa wataweza kuwapa mikataba watu watakaoteuliwa kushiriki katika zoezi la kuwapiga risasi Nguruwe wanaorandaranda mjini humo, kulingana na malipo watakayotaka.
Waliongeza kuwa wale watakaoruhusiwa kuwaua Nguruwe hao watateuliwa mwezi Mei.
Kero la Nguruwe wanaorandaranda mitaani nchini India
Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yamekasirishwa sana na pandekezo hilo la serikali.
‘‘Huu ni unyama na sio suluhu la tatizo la wanyama hao wanaorandaranda mjini,’’alisema Puneet Tripathi, mwasisi wa shirika la kutetea haki za wanyama na mazingira.
‘‘Lazima maafisa waangalie njia nyengine za kusuluhisha tatizo hilo labda kwa kuwahamisha wanyama hao hadi katika mji mwingine,’’ aliongeza bwana Puneet.
Baadhi ya wanaharakati wanasema kuwapiga risasi Nguruwe itakuwa kinyume na sheria za India kuhusu ukatili.
Nguruwe wameonekana kama kero sio mjini humo pekee bali pia katika miji mingine nchini India. Huonekana mara kwa mara wakipekuwa kwenye majaa ya taka wakitafuta chakula.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: