Kwa kupitia njia bunifu ya kupata maoni iliyoendeshwa na Farm Radio International, wakulima 8,891 kote nchini walihojiwa kuhusu uhakika wa kufikia masoko ya ndani.
Hii ni mara ya kwanza kwa wakulima wengi Tanzania kupata fursa ya kutoa maoni yao kwa njia ya simu ambayo ni rahisi na isiyo na gharama.
Ukusanyaji wa maoni uliyoendeshwa ndani ya majuma mawili na kutangazwa na vituo vya redio kupitia vipindi vya ukulima, iliibua mambo yafuatayo:
• 65% hawadhani kama wanafikia masoko ya uhakika kwa ajili ya mazao yao.
• 45% wanadhani ya kuwa mikakati ya kilimo (kupitia misaada na miradi toka nje) imewasaidia kuongeza mavuno ya mazao yao miaka miwili iliyopita. 55% ya wakulima wanadhani misaada na miradi hiyo haikuwasaidia.
• 64% hawadhani kama Tanzania imefanya kiasi cha kutosha kuwasaidia wakulima wadogo kufikia masoko mazuri.
• 44% wanaitaka serikali ya Tanzania iwapatie elimu zaidi kuhusu masoko. 31%wanataka mfumo wa ushuru wa mazao urekebishwe.
• 70% wanakubali kuwa ufikiwaji wa masoko ya uhakika ungeweza kuongeza mavuno ya mazao ndani ya miaka miwili
Matokeo ya maoni hayo yanatolewa leo Dar es Salaam wakati wa hafla yenye ujumbe ‘Kilimo Kinalipa, Jikite.’ Hii ni kampeni ya bara lote la Africa ambayo jamii inawataka viongozi wa nchi za Afrika kufanya mabadiliko na kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya kilimo watakapokutana kwenye kilele cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika mwishoni mwa mwezi huu.
Kilimo Kinalipa, Jikite ni kampeni iliyozinduliwa mahsusi kuadhimisha Mwaka wa Kilimo na Uhakika wa Chakula wa Umoja wa Afrika, na imeandaliwa na taasisi ya ONE, Jukwaa la Wadau wa Kilimo nchini (ANSAF) na Kigoda cha Bill & Melinda Gates, na kuungwa mkono na wasanii kadhaa mashuhuri hapa Tanzania, akiwemo A.Y. na Diamond Platnumz.
Hoja ya Kilimo Kinalipa, Jikite, inayowataka viongozi wa Afrika kuwekeza katika kilimo na kuwasaidia wakulima wadogo imeungwa mkono kwa kutiwa sahihi zipatazo milioni moja.
Akizungumzia matokeo ya maoni hayo, Japhet Emmanuel, Mkurugenzi wa , wa Farm Radio International, Tanzania alisema: “Mwamko wa wakulima kutoka sehemu mbali mbali kushiriki katika kutoa maoni yao ni ishara tosha inayothibitisha kuwa wakulima wanataka kusikilizwa.
Kilimo ni chanzo cha kipato kwa kaya nyingi na ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, lakini cha kushangaza wakulima wanaendelea kukumbwa na changamoto za kupata masoko ya uhakika ya mazao yao.”
Audax Rukonge, Mkurugenzi wa wa ANSAF alisema: “Kilimo ni tumaini la maisha ya baadaye Tanzania na Afrika. Maoni haya yanaieleza serikali nini hasa kinatakiwa kifanyike—kuanzia ngazi ya wakulima wenyewe—ili kuwasaidia wakulima.
Kuwasaidia wakulima kupata uelewa mzuri kuhusu tabia ya masoko na jinsi inavyofanya kazi, na kuwatengenezea mazingira wezeshi—kama vile kurekebisha mfumo wa ushuru wa mazao—ingewasaidia wakulima kulima zaidi, kuongeza kipato chao na uhakika wa chakula na hatimaye kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.”
Naye Dkt. Sipho Moyo kutoka ONE alisema: “Ifikapo 2030, masoko ya chakula barani Afrika yanatazamiwa kukua na kufikia sekta yenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja.
Kwa kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo, viongozi wa Afrika watakuwa wametumia fursa dhahiri kuonesha kuwa wamedhamiria kuondoa moja kwa moja njaa na umaskini.
Waafrika milioni moja tayari wameorodhesha majina yao kuunga mkono hoja hii, na wanasimama na wakulima wadodo wa Tanzania kuwataka viongozi wafanye kitu cha ziada kusaidia kilimo na wakulima wadogo.”
0 comments: