Video: Lampard aanza kuaga Stamford Bridge
Kiungo wa Uingereza Frank James Lampard amesema hana budi kufanya maamuzi magumu ya kuondoka kwenye klabu ya Chelsea na kwenda kusaka maisha mengine nje ya nchi yake.
Frank Lampard amesema imemuuwia vigumu kufanya maamuzi ya kuachana na klabu ya Chelsea ambayo ameitumikia kwa miaka 13 tena kwa mafanikio makubwa.
Amesema anajua kuondoka kwake hakutoathiri jambo lolote ndani ya klabu hiyo ya jijini London, hivyo amewataka mashabiki wake kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho amesisitiza hana budi kuondoka.
Hata hivyo kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35, amesema suala la kuondoka kwenye klabu ya Chelsea katu haliwezi kumuathiri katika maandalizi ya kujiandaa na fainali za kombe la dunia ambapo kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kimeweka kambi mjini Miami nchini Marekani.
Wakati huo huo Frank James Lampard anatarajia kuiongoza timu yataifa ya Uingereza katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Ecuador ambao utachezwa hii leo huko nchini Marekani.
Lampard amesema amefurahishwa na hatua ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza Roy Hodgson kumpa heshima ya kuwa nahodha katika mchezo huo, ambao utakuwa mchezo wa pili wa kujiandaa na fainali za kombe la dunia baada ya kuibanjua timu ya taifa ya Peru mabao matatu kwa sifuri mwishoni mwa juma lililopita.
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza Roy Hodgson amesema kambi ya kikosi chake inaendelea vizuri na ana hakika mchezo wa hii leo utakisaidia kikosi chake kikamilifu katika harakati za kuelekea nchini nchini Brazil.
Amesema hali ya wachezaji wote mpaka sasa ni shwari na ana hakika wote watakwenda nchini Brazil wakiwa na afya njema tayari kwa mapambano ya kurejea historia ya mwaka 1966 ambapo ilikuwa mwanzo na mwisho kwa Uingereza kutwaa ubingwa wa dunia.
0 comments: