Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupanda upya kwa bei za mafuta ya taa, dizeli na petroli ambapo imesema kuwa bei hizo zimepanda juu zaidi ambapo zinatarajia kuanza kutumika leo nchini kote.
Akitangaza kupanda kwa bei hizo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema kuwa bei hizo zimepanda juu zaidi kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la duni hivyo hawana budi kupandisha bei za mafuta hayo.
Alisema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaani petroli, dizeli na mafuta ya taa zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Juni 3 mwaka huu ambapo Julai mwaka huu (leo) bei za rejareja kwa bidhaa hiyo zimeongezeka na petroli sh. 232 kwa lita sawa na asilimia 11.82, dizeli sh. 261 sawa na 14.65 na mafuta ya taa yameongezeka kwa sh. 369 sawa na asilimia 22.75.
“Kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nazo zimeongezeka ambapo ni sh. 232.35 kwa lita sawa na asilimia 12.45, sh. 261.15 kwa lita sawa na asilimia 15.57 na sh.369.41 kwa lita sawa na asilimia 24.32, mabadiliko haya yametokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia,”alisema Bw. Ngamlagosi.
Aidha alisema mabadiliko hayo ni kuendelea kudhoofu kwa thamani ya sh. dhidi ya dola ya Marekani pamoja na mabadiliko ya tozo za Serikali katika mafuta kuanzia Julai mwaka huu na kwamba kwa kulinganisha thamani ya sh. dhidi ya dola kwa machapisho ya bei za Juni na Julai mwaka huu sh. ya Tanzania imepungua thamani kwa sh. 175.11 kwa dola ya marekani sawa na asilimia 8.65.
Mkurugenzi huyo, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008 bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo EWURA itaendeleakuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta ambapo taarifa hizo zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
Aidha EWURA imekanusha taarifa zilizoenea kwenye mitandao kuwa kuna watu watafanya migomo kutokana na kupandishwa kwa mafuta hayo huku wengine wakitishwa kuwa ni lazima waweke mafuta mengi kwenye magari yao mapenda jambo ambalo alisema kuwa siyo kweli badala yake mafuta yapo na ni ya kutosha.
“Tayari tumeongea na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia wale wote waliojihusisha na kutoa taarifa hii kwenye mitandao na kuwachukulia hatua kwani huu ni upotoshaji ambao hautakiwi kufumbiwa macho,”alisema na kuongeza;
“Lakini pia kwa wafanyabiashara ambao wataonekana si waaminifu na kuficha mafuta basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwani tayari tunafuatilia makampuni matano ambao tumewaandikia barua na kuwauliza kuwa ni kwanini wasifungiwe kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo kwenye vituo kutokuwa na mafuta wakati kwenye maghara yao mafuta yapo,”alisema Bw. Ngamlagosi.
Alisema mtu atakayejihusisha na ufichaji wa mafuta faini yake ni sh. milioni 20, jela miaka miwili na kuwataka kutofanya vitendo hivyo ili kuondokana na adhabu hizo.
Kuhusu hali ya mafuta nchini, Mkurugenzi wa Petroli Godwin Samwel, alisema kuwa mafuta yapo ya kutosha ambapo mafuta yaliyopo gharani ni petroli ipo ya siku 12, dizeli siku 12, mafuta ya taa ya siku 97 na mafuta ya ndege yapo ya siku 35 huku akibainisha kuwa yanayoendelea kushushwa bandalini ni Petroli tani 33,800 na dizeli tani 10,500.
0 comments: