Tuesday, 23 August 2016

Yanga wamekuwa walaini kwa TP Mazembe, waaga michuano


Yanga ilipata pigo dakika mbili baada ya kuruhusu goli, Andrew Vicent ‘Dante’ alioneshwa kadi nyekundu na kuiacha Yanga ikicheza pungufu
Safari ya wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi Yanga leo imefikia mwisho kwa kipigo cha mabao 3-1, dhidi ya TP Mazembe.
Yanga imehitimisha safari hiyo kwa kumaliza nafasi ya misho kwenye Kundi A, huku ikijikusanyia pointi nne na sasa inarudi nyumbani kuendelea na msimu mpya wa Ligi ya Vodacom ambayo tayari imeanza wikiendi iliyopita na yenyewe itashuka dimbani Agosti 28 dhidi ya African Lyon.
Yanga iliyowakosa nyota wake sita wa kikosi cha kwanza iliuanza mchezo huo kwa kufanya mashambulizi mengi lakini ilijikuta ikipachikwa bao la kwanza dakika ya 28, kupitia kwa Bolingi, aliyemalizia pasi nzuri ya Ranford Kalaba.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuichanganya Yanga na dakika mbili baadaye ilijikuta ikicheza pungufu baada ya beki wake Andrew Vicent ‘Dante’ kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 30, kwa kumchezea vibaya Kalaba.
Pamoja na kucheza pungufu Yanga walionyesha kupambana na kutengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia huku mshambuliaji wake Amissi Tambwe akikosa msaada kutokana na mbele kubaki peke yake.
Mazembe walirudi kwa kasi kipindi cha pili na katika dakika ya 56, ilipata bao la pili kupitia kwa Kalaba na mshambuliaji huyo aliyeikosa mechi ya Dar es Salaam alifunga bao la pili dakika ya 64 akimalizia pasi nzuri ya Kasusula.
Pamoja na mabao hayo kuingia mfululizo Yanga hawakukata tamaa waliendelea kupambana huku wakifanya mashambulizi ya kustukiza na dakika ya 72 walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi baada ya Amis Tambe kumalizia mpira uliogonga mwamba wa juu ambao ulipigwa na Haruna Niyonzima.
Matokeo hayo yanaipa Mazembe fursa ya kuongoza Kundi A kwa kufikisha pointi 13, na kufuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali huku mshindi wa pili wa kundi hilo akitarajiwa kujulikana baada ya moda mchache katika mchezo ambao Medeama na MO Bejai wanapambana huko Algeria.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: