Thursday, 15 May 2014

DENGUE YAPIGA HODI ARUSHA



Wauguzi Mount Meru waingiwa
hofu, wamsusa mgonjwa
HOMA hatari ya Dengue imeanza kusambaa
katika mikoa mingine nchini, ambapo sasa
imevamia jiji la Arusha.
Dengue, ambayo imeshaua zaidi ya watu watano
mpaka sasa na wengine zaidi ya 450
wakiendelea kupatiwa matibabu katika Jiji la Dar
es Salaam, imezidi kuibua hofu kwa wananchi.
Tayari mkazi wa Maji ya Chai mkoani Arusha,
Frank Nnko (30), amelazwa katika Hospitali ya
Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, akitokea
Hospitali ya Wilaya ya Meru (Patandi).
Hata hivyo, wakati Nnko akifikishwa hospitali
hapo, hali haikuwa shwari kutokana na baadhi
ya wauguzi kushindwa kumpatia huduma kwa
wakati kwa kile walichodai kuogopa
kuambukizwa.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, Nnko
alilazimika kusubiri kwa saa mbili akiwa kwenye
gari la wagonjwa lililomfikisha hospitalini hapo
kusubiri wapate vifaa vya kujikinga na ugonjwa
huo.
Hatua hiyo ilisababisha ndugu na jamaa wa
mgonjwa huyo kulalamikia hatua hiyo huku
wakihoji iwapo ni kweli serikali imesambaza
vifaa tiba vya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela,
alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo na
kuongeza kuwa tayari ameanza kupatiwa
matibabu ikiwa ni pamoja na vipimo.
Alisema vipimo vya mgonjwa huyo vimeletwa
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uthibitisho zaidi.
Mongela alisema mgonjwa huyo alifikishwa
hospitalini hapo jana saa 10 jioni, ambapo baada
ya msuguano mkali wa wauguzi kukwepa kumpa
msaada, baadaye alipokelewa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru,
Omar Chande, alithibitisha kumpokea mgonjwa
huyo na kueleza kuwa, kwa sasa wanachokifanya
na kumpatia tiba mchanganyiko.
“Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo akitokea
Patandi Meru, lakini tunaendelea kumpatia tiba
mchanganyiko, ikiwemo ya malaria, ambayo
alikutwa nayo pamoja na dengue maana hadi
sasa hii homa haina tiba maalumu,” alisema na
kuongeza kuwa hali yake kwa sasa inaendelea
vizuri.
Dengue tishio zaidi Dar
Juzi, serikali iliziagiza Halmashauri za Manispaa
za mkoa wa Dar es Salaam, kusimamia mara
moja upuliziaji dawa katika maeneo yenye
mkusanyiko ili kukabiliana na ugonjwa wa homa
ya dengue.
Imeziagiza Manispaa za Ilala, Temeke na
Kinondoni, kutenga fedha za dharura kwa ajili ya
kupambana na ugonjwa huo.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (SUMATRA), imetakiwa kuandaa
utaratibu wa kupulizia dawa mabasi yote
yaendayo mikoani, meli na treni ili kuepuka
kusambaa kwa ugonjwa huo.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa, Meck
Sadiki, ambapo pia alieleza hatua mbalimbali
zinazochukuliwa na serikali katika kudhibiti
ugonjwa huo.
Ugonjwa huo ni mpya hapa nchini na ulianza
mwishoni mwa Januari, mwaka huu na tangu
ulipothibitika kuwa upo Dar es Salaam, karibu
watu 523 walipimwa.
Kati ya watu hao, 414 walithibitika wana dengue
ambapo Kinondoni walikuwa 342, Temeke 20 na
Ilala 52.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: