Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mtu
kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la kuhakiki
silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya Shortgun na Pistol
zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza
baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa
Mkoa wa Dar es salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la uhakiki
wa Silaha, na ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima
kuhakikisha zinahakikiwa.
Dkt.
Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana
na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu ili kutokomeza kabisa
vitendo hivyo.
"Ni
aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa silaha, ni
aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na wewe
una silaha?" Amehoji Rais Magufuli
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna
Simon Sirro, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono zoezi hilo na
amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika
kwa mafanikio.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti cha Umeya
katika Jiji la Dar es salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata Meya
katika uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala
ya kuendelea kurumbana.
Dkt.
Magufuli amesema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi
huo, ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya
kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
"Mahali
tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali
tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" ameongeza Rais Magufuli
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
Kamanda
wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna CP Simon Sirro kulia
akimkabidhi Silaha aina ya Bastola Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya uhakiki
uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kamanda
wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna CP Simon Sirro kulia
akimkabidhi silaha aina ya shortgun Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya uhakiki
uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiiweka silaha yake vizuri mara baada ya kuhakikiwa Ikulu jijini Dar es
Salaam.
0 comments: