Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia
mwezi April mwaka huu, itaanza kulipa pensheni kwa wazee wote wenye umri
wa kuanzia miaka sabini ili kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi
inayowakabili wazee waishio visiwani humo.
Mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni
moja nukta tano zimetengwa kwa ajili ya malipo ya miezi mitatu ya
pensheni hiyo kabla ya kuisha kwa mwaka huu wa fedha, kipindi ambapo
Baraza la Wawakilishi litapitisha kiwango kipya cha pesa za pensheni kwa
mwaka ujao wa fedha.
Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii
kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Salum Rashid Mohemmed,
amesema hayo leo katika mkutano wa kitaifa ulioandaliwa na asasi ya
HelpAge International tawi la Tanzania, kwa ajili ya kutathmini
utekelezaji wa sheria za kimataifa na za kikanda, za usimamizi na ulinzi
wa haki za wazee ambazo Tanzania kama nchi imeziridhia.
Kwa mujibu wa Bw. Mohammed, takribani
wazee elfu ishirini watanufaikia na mpango huo ambapo kila mmoja
atapatiwa kiasi cha shilingi elfu ishirini kila mwezi huku kiwango cha
pensheni kikitarajiwa kupanda kulingana na hali ya uchumi itakavyokuwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkazi
wa Help Age Tanzania Bw. Smart Daniel, amesema kuna haja ya Tanzania
Bara kuiga mpango huo wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwani wazee
nchini wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi huku sababu kuu ikiwa ni
hatua ya serikali kutosaini sheria ya wazee takribani miaka kumi na tatu
tangu bunge litunge na kuipitisha.
Akinukuu ripoti ya mwaka jana ya hali
ya wazee duniani; Bw. Daniel amesema hali ya wazee nchini sio nzuri
kwani katika ripoti hiyo, Tanzania imeshika nafasi ya tisini na moja
kati ya nchi tisini na sita zilizofanyiwa utafiti.
Aidha, amesema licha ya wazee
kukabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, wao ndio wamekuwa walezi wa kundi
kubwa la wajukuu ambao wengi wao ni watoto yatima, sambamba na kuwa na
jukumu la kuhudumia watoto na wajukuu wao walioathirika kwa ugonjwa
hatari wa ukimwi.
0 comments: